Na Oscar Assenga, MUHEZA

VIKUNDI 29 vya Wanawake,Vijana na Watu Wenye ulemavu wamekabidhiwa Milioni 250 zinazotokana na mikopo asilimia 10 kutoka katika Halmashauri ya wilaya ya Muheza ikiwa ni kuwawezesha kujikwamua kiuchumi wao na jamii zao.

Makabidhiano ya Hundi ya Fedha hizo ilitolewa na Mkuu wa Mkoa wa Tanga Dkt,Balozi Batilda Burian na kushuhudiwa na viongozi mbalimbali wa wilaya ya Muheza akiwemo Mkuu wa wilaya,Mkurugenzi wa Halmashauri,Mwenyekiti wa Halamshauri na Madiwani wa Halmshauri hiyo.

Akizungumza baada ya kukabidhi mikopo hiyo ,Mkuu huyo wa Mkoa aliwaasa wanufaika wa mikopo ya asilimia 10 ya Halmashauri kuitumia kwa uangalifu ili kuweza kujikwamua kiuchumi pamoja na kuhakikisha wengine nao wananufaika na fursa hizo.

Alisema kwamba dhamira ya Rais Dkt Samia Suluhu ni kuona mikopo hiyo inawafikia wahitaji bila kuwepo kwa vikwazo vya aina yoyote kupitia mfumo wa mtandao bila kuhitaji kumjua mtu .

Aidha alitoa wito kwa vijana kujitokeza kwa wingi kuchangamkia fursa za uwepo wa mikopo hiyo ili waweze kujikwamua kiuchumi.

“Tumekubaliana kuandaa kongamano la vijana litakalowakutanisha maafisa maendeleo ya jamii na wadau wa mikopo kwa lengo la kuwaelimisha juu ya mchakato mzima wa kuipata na jinsi ya kuunda vikundi imara”Alisema

Mkuu huyo wa mkoa alisema lengo ni kuhakikisha kila kijana anakuwa na uelewa hatua za kuomba mikopo na kutumia fursa zilizopo.

Awali akizungumza Mkuu wa wilaya ya Muheza Ayoub Sebabili alisema kwamba mikopo iliyozinduliwa ya asilimia 10 ,wanawake asilimia 4,vijana 4 na walemavu 2 huku akimpongeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Muheza Dkt Jumaa Mhina na menejimentii ya halmshauri kwa kuratibu vizuri mikopo na kuwafikia walengwa.

Aliwaomba wanufaika wa mikopo hiyo watoa ushirikiano kwenye marejesho ili kuweza kutoa nafasi watu wengine kupata mikopo kwa lengo la kukuza kipato na kujikwamua kiuchumi.





“Tunaopokea mikopo hii tutoe ushirikiano wakati wa marejesho kwa sababu utapelekea mfuko wa mikopo uweze kuwa endelevu na kuwafikia watu wengine na hivyo kuondoa umaskini kwa mtu mmoja mmoja na wengine kunufika nayo”Alisisitiza



Naye kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmshauri ya Muheza Dkt Jumaa Mhina alimpongeza Mkuu huyo wa wilaya akieleza kwamba ndio muhimili wa halmashauri kuhakikisha asilimia 10 inatoka na kufikia vikundi hivyo.


Dkt Jumaa alisema kwamba wameweka mkazo kwa vikundi vyote lakini hususani kwa vijana ambao siku za nyuma walikwa wanawatafuta kwa tochi hivyo sasa watawafuata vijana walipo ili kuwaibua waweze kuunda vikundi na hivyo kunufaika na mikopo asilimia 10 ikiwa ni sehemu ya kutengeneza ajira .



Share To:

OSCAR ASSENGA

Post A Comment: