Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira imekoshwa na miradi mbalimbali inayotekelezwa na Wizara ya Maji na kuwataka wananchi zaidi ya laki tano wanaotegemea kunufaika na Mradi wa Maji  wa Miji 28 Rujewa kujiandaa kupata huduma ya uhakika ya majisafi kutoka katika mradi huo mwezi Desemba 2026.

Mwenyekiti wa kamati Mhe. Jackson Kiswaga (Mb), na wajumbe wa kamati hiyo wamekagua miradi mbalimbali ukiwamo mradi wa Miji 28 Rujewa ambao utekelezaji umefika asilimia 80, ukitarajiwa kuzalisha maji lita za ujazo milioni 40 kutoka mahitaji ya lita milioni 32 kwa siku hivyo huduma ya maji kupatikana kwa asilimia 100.

Thamani ya mradi ni takriban shilingi bilioni 105.7 na chanzo chake ni  maji ya mto Mbarali Mradi utanufaisha wakazi wa  Rujewa (Mbeya), Wanging'ombe na Makambako (Njombe).

Eneo jingine lililokaguliwa na kamati ni chanzo cha maji cha bonde la Usangu kilichanzishwa mwaka 2010 ambapo Mhe. Kiswaga ameelekeza zoezi la kuotesha miti rafiki lifanyike ndani ya mita 60 za chanzo ili kuhakikisha maji yanakuwepo katika misimu yote ya mwaka.

Sanjari na hilo,  kamati imekagua mradi wa Kuimarisha Mbinu za Asili za Jamii za Utunzaji wa Vyanzo vya Maji Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi, kazi ambayo wananchi wamewezeshwa na Serikali kupata kisima kirefu cha mita 228 kinachohudumia vitongoji vitano, na mabirika 10 ya kunyweshea mifugo ili kulinda vyanzo vya maji kupitia vikundi vilivyowezeshwa 30.

Mwenyekiti wa Kamati Mhe. Kiswaga kuhusu kulinda vyanzo amewataka wananchi kwa ushirikishwaji katika miradi wahakikishe fedha inayotolewa na serikali inatumika kuwezesha uendelevu wa miradi ya maji.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji Mhandisi Mwajuma Waziri katika ukaguzi huo amesema Wizara ya Maji inahakikisha rasilimali za maji zinanufaisha jamii yote, wakiwamo wafugaji, hivyo ushirikiano na sekta nyingine unazidi kuwa imara katika kutoa huduma.

Share To:

OSCAR ASSENGA

Post A Comment: