Mfanyabiashara na Mwenyekiti wa Taifa Group, Rostam Azizi, ametoa rai kwa Serikali na wadau mbalimbali kuweka maslahi mbele katika suala la uwezeshaji Watanzania ili kuwawezesha kumiliki uchumi wa nchi, kama ambavyo Wizara ya Madini imeanza kutekeleza na kusimamia sheria za kuwawezesha Watanzania kushiriki na kunufaika na madini kupitia kanuni ya maudhui ya ndani ya ushirikishwaji wa Watanzania katika mnyororo wa thamani wa madini (Local Content).

Akizungumza katika hafla ya utoaji wa Tuzo za Umahiri katika Sekta za Ujenzi na Madini (African Construction and Mining Excellence Awards – ACAMEA) 2026, iliyofanyika jijini Dar es Salaam, ambapo alikuwa mgeni rasmi, Rostam Azizi alisema Tanzania ina fursa nyingi, mojawapo zikiwa ni madini na ujenzi wa miradi mikubwa ya miundombinu.

Alisema nchi ina idadi kubwa ya vijana wenye uwezo na ari ya kufanya kazi, hivyo wasipojengewa mazingira mazuri, fursa hizo hazitanufaisha vijana wa Kitanzania wala kujenga makampuni imara nchini.
Rostam Azizi

Alisema jukumu la uwezeshaji Watanzania si la Serikali pekee, bali linahusu sekta binafsi, taasisi za fedha, wakandarasi na wataalamu wa ndani.

“Serikali ina nafasi ya kuwa na sera wezeshi na kutengeneza mazingira yanayotoa fursa sawa kwa wote, Taasisi za fedha zina nafasi ya kuwezesha upatikanaji wa mitaji. Na kampuni zetu zina wajibu wa kujenga uwezo, kuzingatia ubora na kutekeleza kazi kwa uadilifu” ,alisema.

Azizi alisema Watanzania hawapaswi kuridhika kujenga barabara bila kujenga uwezo wa wakandarasi wao, kujenga reli bila kujenga kampuni zenye uwezo wa kutekeleza miradi mikubwa au kuchimba madini bila kujenga uwezo wa Watanzania kumiliki sehemu kubwa zaidi ya uchumi unaotokana na rasilimali hizo.

“Tunaposherehekea washindi wa ACAMEA leo, tusherehekee pia uwezo wao wa kufanya makubwa zaidi huko mbeleni. tujiulize sisi, kama Serikali, wawekezaji na viongozi wa sekta hizi, tunafanya nini kuhakikisha uwezo huo hauishii hapa.Miundombinu tunayojenga leo itakuwa urithi wa vizazi vijavyo. Lakini urithi mkubwa zaidi utakuwa uwezo wa Watanzania kuujenga, kuumiliki na kuuendeleza uchumi wao wenyewe”,alisisitiza.

Alisema kuna maswali ambayo Watanzania wanapaswa kujiuliza kupitia miradi mikubwa inayojengwa nchini, ikiwemo barabara, reli, madaraja, mabwawa na miundombinu mingine mikubwa.
"Tunajenga kampuni kubwa za Kitanzania? Na fedha nyingi kutumika kujenga miradi hiyo Ni kampuni ngapi za Kitanzania zimekua? Ni wakandarasi wangapi wamejenga uwezo mpya? Na ni utaalamu gani utabaki nchini kwa ajili ya miradi ya baadae? Na kusisitiza kuwa maendeleo hayatokani tu na kukamilisha miradi bali ni pamoja na kujenga uwezo wa Watanzania kutekeleza miradi hiyo wenyewe".

Azizi alihoji kwa nini sekta nyingine zisichukue hatua kama Wizara ya Madini katika kuwawezesha Watanzania.

"Kama Wizara ya Madini imethubutu kuchukua hatua za makusudi za kuwalinda na kuwawezesha Watanzania akisema .."Kwa nini tusifanye hivyo hivyo katika sekta ya ujenzi na sekta nyingine za uchumi wetu? na kusema kuwa madini sio suala la mapato na ajira tu, bali pia ni suala la kujenga kampuni imara za Kitanzania, viwanda, teknolojia, wataalamu na kukuza mitaji ili kuendelea kuzalisha thamani hata baada ya madini kuisha".

Alisema thamani ya madini haipo tu kwenye madini yanayochimbwa ardhini, bali pia kwenye huduma na shughuli mbalimbali zinazozunguka sekta hiyo.

“Thamani ya madini haipo tu kwenye kile tunachokichimba ardhini. Ipo pia kwenye uhandisi, mitambo, teknolojia, usimamizi na biashara zinazozunguka shughuli za uchimbaji.Hizi ni fursa ambazo Watanzania wanapaswa kuzitumia kujenga uwezo wa kampuni zao”,alisema.

Aliipongeza Serikali kupitia Wizara ya Madini kwa hatua ilizochukua kuimarisha ushiriki wa Watanzania katika sekta hiyo kupitia sera, sheria na kanuni za ushiriki wa Watanzania katika mnyororo wa uchimbaji madini, zikiwemo marekebisho ya mwaka 2025, ambayo yanaendelea kuongeza fursa kwa kampuni za Kitanzania kushiriki katika shughuli za uchimbaji na huduma mbalimbali zinazohusiana na migodi.
Azizi alitoa rai ya kuondokana na dhana ya kuyaona makampuni ya Kitanzania kuwa hayana uwezo wa kufanya kazi kubwa, akieleza kuwa kampuni haikui kwa kutamani ikue tu, bali inakua kwa kupata kazi, kujenga uzoefu, kukusanya mtaji na kuwekeza. Hata hivyo, alisema ili kampuni ipate kazi, ni lazima kuwe na mtu anayeamini kuwa inaweza kufanya kazi hiyo.

"Lazima kwanza kuwe na mtu anayeamini kwamba inaweza kuifanya kazi hiyo na hapa ndipo kuna tatizo kwa kuwa Watanzania hatuaminiani",alisema.

Alisisitiza kuwa si kila kampuni ya Kitanzania ina uwezo wa kutekeleza kila mradi mkubwa, kwa kuwa miradi hiyo inahitaji utaalamu, mitaji, teknolojia na usimamizi wa hali ya juu. Hata hivyo, alisema hilo halimaanishi kuwa hakuna kampuni za Kitanzania zenye uwezo.

“Si kila kampuni ya Kitanzania ina uwezo wa kutekeleza kila mradi mkubwa. Miradi mikubwa inahitaji utaalamu, mitaji, teknolojia na usimamizi wa hali ya juu. Hilo halina ubishi. Lakini hilo halimaanishi kwamba hakuna kampuni za Kitanzania zenye uwezo. Na pale ambapo uwezo haujatosha, tunapaswa kuwa na mkakati wa kuujenga, kama ni mitambo, inaweza kununuliwa au kukodishwa. Wataalamu wanaweza kuajiriwa. Teknolojia inaweza kupatikana. Ubia unaweza kuundwa. Uzoefu unajengwa kwa kufanya kazi,hatuwezi kuendelea kusema kwamba wakandarasi wetu hawana uwezo, wakati hatuwapi fursa za kuujenga uwezo huo. Uzoefu haupatikani kwa kusubiri. Unapatikana kwa kufanya kazi",alieleza.

Kuhusu upatikanaji wa wakandarasi wa kutekeleza miradi mikubwa nchini, Rostam alishauri kuwa uwezo wa mkandarasi haupaswi kupimwa kwa jina, uraia wake au lugha anayoizungumza, bali kwa kuzingatia wataalamu wake, uwezo wake wa kifedha, rekodi ya utekelezaji, usalama na ubora wa kazi zake.

"Na tusimdharau mkandarasi wa Kitanzania kwa sababu tu anazungumza Kiswahili na kuondokana na dhana kuwa mkandarasi kutoka nje anao uwezo mkubwa zaidi kwa sababu tu anazungumza lugha ya kigeni na kampuni zote na hapa, ninaomba nisieleweke vibaya",alisema.
Alisema hapingani na kampuni za kigeni kwa kuwa zina nafasi yake, huku utaalamu na teknolojia zinazoleta nchini zikihitajika. Alifafanua kuwa anachopinga ni dhana kwamba kampuni ya kigeni ina uwezo kwa sababu ni ya kigeni, na kampuni ya Kitanzania haina uwezo kwa sababu ni ya Kitanzania.

Aidha, alisema Serikali inatumia fedha nyingi kujenga miundombinu, lakini sehemu kubwa ya mikataba mikubwa inaendelea kutekelezwa na kampuni za kigeni, huku wakandarasi wengi wa ndani wakibaki na kazi ndogo ndogo.

Alisema hali hiyo inasababisha wakandarasi wa Kitanzania kuendelea kudumaa, huku pia wakikabiliwa na changamoto ya kucheleweshewa malipo baada ya kufanya kazi, jambo linaloweka kampuni zenye uwezo katika hatari ya kufilisika.

Azizi alishauri kuwa ili kampuni za Kitanzania ziimarike, kunahitajika sera na mfumo wa kisheria unaowapa wakandarasi wa ndani fursa za kweli, unaolinda ushindani wa haki na kuwajengea uwezo wa kutekeleza miradi mikubwa.

"Tusijenge uchumi wa dola trilioni moja ambao vijana wetu watakuwa watazamaji.Tujenge uchumi ambao vijana hawa watakuwa washiriki, viongozi na wamiliki. Kwa sababu mustakabali wa uchumi wetu hautategemea tu kiwango cha uwekezaji tutakachovutia, bali pia uwezo wa Watanzania kushiriki, kuongoza na kumiliki sehemu ya uchumi huo",alisisitiza.

Azizi aliwapongeza washindi wa tuzo za ACAMEA na kuitaka tuzo hiyo iendelee kuwa jukwaa linalounganisha kampuni zenye uwezo na fursa za miradi, taasisi za fedha, teknolojia na washirika wanaoweza kuzisaidia kukua.

"Ningependa kuona katika miaka ijayo kampuni tunazozitambua hapa leo zikiwa zimekua, zikiwa na mitaji mikubwa zaidi, zikiwa zimeajiri Watanzania wengi zaidi na zikiwa na uwezo wa kutekeleza miradi mikubwa zaidi",alisema.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Masoko na Uhamasishaji Mitaji wa Chama cha Wadhamini Sekta ya Madini Tanzania (TAMISA), Dkt. Sebastian Ndege, alisema hafla hiyo imehusisha wadau mbalimbali wakiwemo taasisi za madini, taasisi za fedha na wadau wengine, ikiwemo Taifa Group, NMB, Clouds Media, TPSF na Blue Coast.

Dkt. Ndege alisema hafla hiyo imehusisha sekta mbili ambazo ni sekta ya madini na sekta ya ujenzi.

"Madini yanatoa rasilimali na ujenzi unatoa rasilimali hizo, tunapoelekea ubora huu, tunasherehekea yote hayo," alisema.


Share To:
Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

Post A Comment: