Na Mwandishi wetu- IRINGA
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu Mhe. Ummy Nderiananga amewataka watu wenye ulemavu kutumia mikopo inayotolewa na Serikali kama fursa ya kujikwamua kiuchumi na kubadili maisha yao, badala ya kuichukulia kama msaada au hisani.
Naibu Waziri aliyasema hayo katika Ofisi za Mkoa wa Iringa, wakati wa ziara yake ya kutoa elimu kwa watu wenye ulemavu kuhusu fursa mbalimbali zinazopatikana kwa lengo la kuwawezesha kiuchumi na kijamii.
Amesemalisema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuweka mazingira wezeshi kwa watu wenye ulemavu kupata mikopo na fursa nyingine za kiuchumi, huku akibainisha kuwa kiasi kikubwa cha fedha tayari kimetolewa kwa wanufaika nchini.
“Hadi sasa watu wenye ulemavu Nchi nzima wameshakopa shilingi Bilioni 26.8 huvyo tunapaswa kushukuru na kuipongeza Serikali kwa mikakati mizuri kuhakikisha Kundi hili linafikiwa na sisi kama watu wenye ulemavu tuchangamkie fursa hihi ya mikopo tujiinue kiuchumi na tuwe waaminifu kurejesha ili kuwawezesha na wengine,”Alieleza Mhe. Ummy.
Mhe. Ummy Alieleza kwamba ongezeko hilo ni ishara kuwa watu wenye ulemavu wameanza kutambua na kutumia fursa zinazotolewa kwa ajili ya kuanzisha na kuendeleza shughuli za kiuchumi, hivyo kuwataka kuendelea kujitokeza na kutumia fursa hizo .
"Mafanikio ya baadhi ya watu wenye ulemavu waliopata mikopo yanapaswa kutumika kama mfano na kuwahamasisha wengine kuchangamkia fursa hii ya mikopo kwani wapo wenye ulemavu wengi wamenufaika hatimaye kupungua wimbi la utegemezi katika familia hata Taifa," Alisisitiza.
Aidha Waziri Ummy aliitaka Halmashauri ya Manispaa ya Iringa kujitathmini katika utoaji wa mikopo kwa watu wenye ulemavu akibainisha kuwa kiwango kilichotolewa katika manispaa hiyo
bado ni kidogo ikilinganishwa na mahitaji yaliyopo huku akiwapongeza watu wenye ulemavu wanaofanya shughuli zao kama vile kiwanda cha kufyatua matofali Kata ya Nduli, duka la jumla la mahitaji ya nyumbani, mnufaika wa mikopo aliyenunua bajaji ya baishara na wafanyabiashara wadogo katika Halmashauri ya Manispaa ya Iringa.
“Serikali za mitaa zinapaswa kuhakikisha fursa za mikopo zinawafikia walengwa, huku wakitenga pia maeneo maalumu ambayo watu wenye ulemavu watafanya shughuli za uzalishaji na biashara biashara zao bila kusumbuliwa,” Alibainisha.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Mhe. Benjamini Sitta alisema Serikali imefanya jitihada kubwa kuhakikisha inatatua changamoto ya mikopo kwa wenye ulemavu kutoka utaratibu wa kukopa kwa vikundi wa awali hadi mtu mmoja mmoja.
Awali akitoa taarifa ya Halmashauri ya Manispaa ya Iringa ya Utoaji wa mikopo kwa vijana, wanawake na wenye ulemavu kwa kipindi cha mwaka 2024/2025 hadi 2025/2026, Afisa Maendeleo ya Jamii ambaye ni Mratibu wa mikopo Bi. Sunday Mtamakaya alieleza kuwa vikundi 183 vimepatiwa mikopo wakiwemo wanawake, vijana na wenye ulemavu.
“ Halmashauri imefanikiwa kuwawezesha wenye ulemavu mitaji, wana vikundi kuboresha hali za maisha yao na baadhi ya wanavikundi kuwaajiri watu wengine katika biashara zao. Licha ya mafanikio hayo bada ya kurejeshwa utaratibu wa mikopo bado kuna changamoto ya baadhi yao kushindwa kuejesha mikopo hiyo kwa uaminifu,” Alisema Afisa Maendeleo huyo.
Naye Mnufaika wa mikopo hiyo mwenye ualbino Bwa. Issa Iddi Sogoi ambaye anamiliki duka la jumla la mahitaji ya nyumbani katika Halmashauri hiyo alimshukuru Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna anavyoonyesha upendo, kujali na kuwaunga mkono watu wenye ulemavu kupitia mikopo hatua inayomsaidia kumudu mahitaji ya familia na kujiongezea kipato ambapo pia ametoa ajira kwa vijana wengine.












Post A Comment: