Meneja wa Usajili wa Bidhaa na Majengo wa TBS, Bw.Habakuki Kalebo,akiwasilisha mada wakati wa kikao kilichoandaliwa na BRELA cha Maafisa Biashara pamoja na Wakuu wa Idara za Viwanda na Biashara kinachofanyika kwa siku mbili jijini Dodoma.
Na.Mwandishi Wetu-DODOMA
Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limesisitiza umuhimu wa kusajili maeneo yote yanayohusika na uuzaji, usambazaji na uhifadhi wa bidhaa za chakula na vipodozi, likieleza kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kuhakikisha wananchi wanapata bidhaa salama na bora, kulinda afya zao.
Meneja wa Usajili wa Bidhaa na Majengo wa TBS, Bw.Habakuki Kalebo, amesema hayo wakati wa kikao kilichoandaliwa na BRELA cha Maafisa Biashara pamoja na Wakuu wa Idara za Viwanda na Biashara, akieleza kuwa TBS inashirikiana na Ofisi ya Rais–TAMISEMI kupitia mamlaka za serikali za mitaa katika kusimamia usajili wa maeneo hayo.
Kalebo amesema usajili huo unalenga kuhakikisha bidhaa zinazouzwa, kusambazwa au kuhifadhiwa ni salama, bora na zimethibitishwa na TBS, huku mazingira yanayotumika kuhifadhi na kuuza bidhaa yamekidhi masharti ya usalama na usafi. Amesema kwa bidhaa za chakula, hatua hiyo inasaidia kuzuia uchafuzi kwa kuhakikisha chakula hakihifadhiwi au kuchanganywa na bidhaa nyingine zinazoweza kuhatarisha ubora wake.
Aidha, amesema usajili huo unasaidia kudhibiti usalama wa vipodozi vinavyoingizwa sokoni, kwa kuhakikisha havina viambata vyenye madhara kwa watumiaji. Ameongeza kuwa ukaguzi katika maeneo hayo pia husaidia kubaini na kuondoa bidhaa zilizomaliza muda wake kabla hazijawafikia wananchi, hivyo kupunguza hatari zinazoweza kujitokeza kutokana na matumizi ya bidhaa zisizofaa.
"Mfumo wa usajili pia una umuhimu katika ufuatiliaji wa bidhaa sokoni, kwani pale changamoto inapojitokeza, TBS inaweza kubaini bidhaa husika zilipo, kiasi kilichopo na kuchukua hatua za haraka za kuziondoa sokoni. Amesema utaratibu huo unaimarisha udhibiti wa bidhaa na kuongeza uwezo wa Serikali kulinda afya na usalama wa wananchi."amesema Bw.Kalebo
Amesema ushirikiano kati ya TBS, Maafisa Biashara na Mamlaka za serikali za mitaa ni muhimu katika kuhakikisha wafanyabiashara wanaelewa na kutekeleza matakwa ya Sheria na Viwango vya bidhaa.
Kalebo amesisitiza kuwa ulinzi wa afya ya wananchi unapaswa kuwa sehemu muhimu ya usimamizi wa biashara, akieleza kuwa mtu mwenye afya njema ana uwezo mkubwa wa kushiriki katika shughuli za uzalishaji na kuchangia uchumi wa taifa.
Amesema matumizi ya bidhaa salama hupunguza hatari za magonjwa na gharama za matibabu, hivyo usajili na udhibiti wa maeneo ya biashara ya chakula na vipodozi ni hatua muhimu katika kulinda afya ya jamii na kuongeza tija ya Taifa.


Post A Comment: