Katibu Mkuu Ofisi ya Rais – Mipango na Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Mipango, Dkt. Tausi M. Kida, amesema ushirikiano kati ya Serikali, Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) Tanzania na wadau mbalimbali ni muhimu katika kugeuza ubunifu, teknolojia na utafiti kuwa chachu ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Dkt. Kida amesema hayo kuelekea Wiki ya Ubunifu Tanzania 2026, inayotarajiwa kufanyika Agosti 31 hadi Septemba 4, 2026 katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam.

Amesema jukwaa hilo litasaidia kuunganisha mawazo bunifu, utafiti, teknolojia, sera, mitaji, masoko na uwekezaji, ili kuchochea suluhisho zenye kuongeza tija, kuzalisha ajira na kuboresha maisha ya wananchi.
“Hatuhitaji ubunifu unaobaki katika mawazo au maabara. Tunahitaji kuugeuza kuwa bidhaa, huduma na suluhisho zinazoongeza tija, kuzalisha ajira, kuvutia uwekezaji na kuboresha maisha ya wananchi,” amesema Dkt. Kida.
Aidha, Amesema ushirikiano wa Serikali, sekta binafsi, taasisi za elimu na utafiti, wabunifu, wajasiriamali, wawekezaji na washirika wa maendeleo utakuwa muhimu katika kujenga mazingira yatakayowezesha mawazo bunifu kufikia hatua ya utekelezaji na soko.
Wiki ya Ubunifu Tanzania 2026, yenye kaulimbiu “Kutoka Kwenye Matarajio hadi Mabadiliko; Kutumia Ubunifu katika Kuelekea Tanzania yenye Ustawi wa Pamoja,” itajumuisha mijadala ya kisera, maonesho ya ubunifu, shughuli za vijana na majadiliano ya uwekezaji.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Mhe. Prof. Kitila Alexander Mkumbo anatarajiwa kuzindua Jukwaa hilo, litakalohusisha mjadala wa Mawaziri kuhusu Ubunifu na Utekelezaji, utakaojadili namna ubunifu na teknolojia vinavyoweza kuimarishwa katika mipango na utekelezaji wa maendeleo ya Taifa.
Unaweza kujisajili sasa kupitia https://summitpoint.co.tz/events/iwtz-2026






Post A Comment: