Na: OWM - TAMISEMI
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) imeanza rasmi vikao vyake jijini Dodoma kwa kukutana na watendaji wa Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, kujadili utekelezaji wa shughuli za Serikali, hususan miradi ya miundombinu na utoaji wa huduma kwa wananchi, ikiwa ni sehemu ya maandalizi kuelekea Mkutano wa Nne wa Bunge unaotarajiwa kuanza Agosti 25, 2026.
Katika kikao hicho, Kamati imepokea na kujadili taarifa ya Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kuhusu ukarabati wa barabara zilizoharibiwa na mvua za masika nchini, pamoja na maendeleo ya ujenzi wa miundombinu ya BRT na mpango wa kuboresha huduma za usafirishaji zinazotolewa na UDART.
Katika vikao hivyo, Kamati pia inatarajia kupitia masuala mbalimbali yanayohusu utoaji wa huduma kwa wananchi, ikiwemo uimarishaji wa huduma za maji na lishe shuleni, utunzaji wa mazingira, ujenzi wa viwanja vya michezo pamoja na ajira za walimu wa michezo katika shule za msingi na sekondari.
Aidha, ratiba ya Kamati inaonesha kuwa itajadili masuala ya elimu, afya na mazingira, ikiwemo ujenzi wa shule na miundombinu yake, mikakati ya kukabiliana na viuadudu katika halmashauri, pamoja na mahitaji ya walimu na maandalizi ya utekelezaji wa mabadiliko ya mtaala wa elimu.












Post A Comment: