Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo (WMA) Alban Kihulla ametuma ujumbe wa shukrani na pongezi kwa wafanyakazi wa Wakala hiyo, siku ya maadhimisho ya siku ya Mei Mosi, 2026.

Katika Andiko hilo, Mtendaji Mkuu ameielezea siku ya Mei Mosi kuwa ni sehemu ya kutambua mchango mkubwa wa wafanyakazi hao katika kujenga uchumi imara kupitia matumizi sahihi ya Vipimo vilivyo katika usahihi unaokubalika kimataifa.

"Ninajivunia kujituma kwenu, uadilifu, na weledi mnaouonesha kila siku katika uhakiki na ukaguzi wa Vipimo pamoja na ukaguzi wa bidhaa zilizofungashwa. 

Kazi yenu ina mchango mkubwa katika kuimarisha biashara yenye haki, kuongeza imani kwa walaji, na kukuza maendeleo ya taifa letu."

Aidha, ameongeza kuwa katika kipindi hiki cha mabadiliko ya teknolojia na ukuaji wa sekta mbalimbali, anawiwa zaidi kuwapongeza kwa kuendelea kujifunza, kuboresha ufanisi, na kuendana na mahitaji mapya ya kazi.

Amewasisitiza kuendelea kushikamana, kudumisha nidhamu ya kazi, na kuzingatia maadili ya utumishi wa umma.

Kiulla ameweka bayana kuwa Uongozi wa Wakala unatambua na kuthamini mchango wa wafanyakazi, na utaendelea kuboresha mazingira ya kazi ili kuwawezesha  kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi.

Share To:

Post A Comment: