Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) linaendelea kuhimiza ushiriki wa wadau mbalimbali katika uhifadhi na usimamizi wa mazingira, likieleza kuwa mafanikio katika sekta hiyo yanategemea ushirikiano wa wananchi, taasisi za umma, sekta binafsi na washirika wa maendeleo.
Kupitia ushiriki wake katika Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma 2026 yanayofanyika katika Viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma, Baraza linaendelea kutoa elimu ya mazingira kwa wananchi na kuonesha mchango wa kila mdau katika kulinda na kuhifadhi mazingira kwa maendeleo endelevu.
Katika banda la NEMC, wananchi na wadau wa mazingira wameendelea kupata elimu kuhusu wajibu wao katika kulinda mazingira, matumizi endelevu ya rasilimali, usimamizi wa taka, upandaji na utunzaji wa miti pamoja na umuhimu wa kuzingatia sheria na kanuni za mazingira katika shughuli za maendeleo.
Hali hiyo imeonesha kuwa mafanikio ya sekta ya mazingira yanategemea ushirikiano wa wadau wote bila kujali sekta wanazotoka.
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Meneja wa Kanda ya Kati NEMC, Bw. Novatus Mushi, amesema mazingira ni suala mtambuka linalogusa nyanja zote za maendeleo, hivyo mafanikio katika uhifadhi wake yanahitaji uwajibikaji wa pamoja kutoka kwa kila mwananchi.
Amesema banda la NEMC limeendelea kuwa jukwaa la kuonesha mafanikio yaliyopatikana katika miaka 40 tangu kuanzishwa kwa Baraza, sambamba na kuelimisha wananchi kuhusu huduma mbalimbali za mazingira na mifumo ya kidijitali inayorahisisha upatikanaji wa huduma hizo.
NEMC inaendelea kutumia maadhimisho hayo kama fursa ya kuimarisha uelewa wa umma kuhusu masuala ya mazingira na kuhamasisha matumizi endelevu ya rasilimali za Taifa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.









Post A Comment: