Articles by "WAKALA WA VIPIMO"
Showing posts with label WAKALA WA VIPIMO. Show all posts




 Na WMA - MWANZA


 Wakala wa Vipimo (WMA) umesisitiza kuwa ni rafiki wa muuzaji na mnunuzi na kwamba sheria ya vipimo haikuundwa kuwakomoa wafanyabiashara bali kuwasaidia kufanya biashara ya haki.

 Kauli hiyo imetolewa leo Septemba 4, 2026 katika Siku ya Nane ya Maonesho ya 21 ya Biashara ya Afrika Mashariki yanayoendelea katika Uwanja wa Furahisha jijini Mwanza.

Wakiizungumza kwa nyakati tofauti na wageni waliotembelea banda la WMA, Wataalamu wa Wakala wamesema lengo la uhakiki wa vifaa vya vipimo ni kulinda pande zote mbili.

"Muuzaji akitumia kipimo sahihi anajenga imani kwa mteja wake na kupata soko la uhakika. Na mlaji naye anapata thamani kamili ya fedha yake. Hapa hakuna mshindi na mshindwa. Sheria ya Vipimo ni msaada, sio adhabu" wamewaeleza wananchi.

Katika siku ya nane ya maonesho hayo, banda la WMA limeendelea kuwa kivutio kwa wafanyabiashara, wazalishaji na wananchi wa kawaida ambapo Wataalamu wameendelea kutoa elimu ya vipimo hususan jinsi ya kutambua vipimo halali pamoja na umuhimu wa kuhakiki vipimo mbalimbali ili kuepuka hasara katika biashara. 

WMA imesema ushiriki wake katika maonesho hayo ni sehemu ya mkakati wa kusogezwa kwa huduma kwa umma na kusikiliza changamoto za moja kwa moja kutoka kwa wadau. 

Wakala wa Vipimo umewahakikishia wananchi kuwa unaendelea kutoa huduma za uhakiki wa haraka katika Ofisi zao zilizopo mikoa yote ya Tanzania Bara na umewakaribisha kuendelea kutembelea banda lao katika Maonesho hayo hadi Septemba 6, 2026 yatakapofungwa.

 


Na WMA - MWANZA

 Meneja wa Wakala wa Vipimo (WMA) Mkoa wa Geita, Bi. Eva Ikula amesema usimamizi wa matumizi sahihi ya vipimo unaofanywa na WMA umewezesha bidhaa za Tanzania kuaminiwa na kukubalika zaidi katika soko la kimataifa.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Agosti 31, 2026 katika banda la WMA wakati wa Maonesho ya Biashara ya Afrika Mashariki yanayoendelea katika Viwanja vya Furahisha jijini Mwanza, Bi. Ikula amesema mojawapo  ya sababu kubwa ya bidhaa za Tanzania kukubalika katika soko la kimataifa ni uhakika wa vipimo.

"Kilo yetu ni kilo ya Kenya, ya India, na ya Ujerumani pia. Hiyo ndiyo nguvu ya matumizi ya vipimo sahihi."

Amesema WMA inaendelea kutoa elimu kupitia kampeni mbalimbali ili kujenga uelewa kuwa "Kipimo sahihi ni pasipoti ya bidhaa yako kuingia soko lolote duniani."

Amebainisha kuwa wanunuzi wa kimataifa wanaiamini Tanzania kwa sababu WMA  inatumia mfumo mmoja wa kimataifa wa vipimo - SI Units.

"Matokeo yake ni rahisi. Mkataba unapotiwa saini London, Beijing au Johannesburg, wanajua kilo ya Tanzania ni sawa na kilo yao," amesema.

Amehitimisha kwa kusema WMA haijali tu kilo na lita bali inajenga imani.

" Tunapouza kwa kipimo sahihi, tunauza kwa heshima. Na dunia inaheshimu wale wanaouza kwa heshima."

Maonesho ya Biashara ya Afrika Mashariki yalianza Agosti 28 na yanatarajiwa kuhitimishwa Septemba  6, 2026 yakiongozwa na kaulimbiu isemayo "Usalama na Amani ni Kichocheo cha  Biashara na Uwekezaji".





 


Banda la Wakala wa Vipimo (WMA) limeendelea kuvutia makundi mbalimbali ya wananchi katika Maonesho ya Biashara ya Afrika Mashariki yanayoendelea katika Viwanja vya Furahisha jijini Mwanza, ikiwa ni siku ya tatu, Agosti 30, 2026.

Makundi hayo yameonesha kuvutiwa na elimu ya vipimo tofauti tofauti.

Wakiwa bandani hapo, wengi wa wanafunzi na vijana wameonesha kuvutiwa zaidi na elimu ya matumizi  ya mizani za kielektroniki na pampu za kupimia mafuta.

 Wamesema elimu hiyo inawapa uelewa wa kuwa mabalozi wa vipimo shuleni na majumbani mwao huku wengine wakidai ndoto yao ni kuwa Maafisa Vipimo wa baadae.

Kwa upande wa akina mama wajasiriamali, wengi  wamejikita kujifunza kuhusu matumizi sahihi ya mizani  inayotumika masokoni na waliuliza maswali mengi kuhusu namna ya kutambua ujazo wa mtungi wa gesi ya kupikia wanapoenda kununua.

 Wengi wameipongeza WMA kwa kuwaelimisha jinsi ya kuepuka hasara na kuhakikisha mteja anapata haki yake.

Askari na wazee waliotembelea Banda la WMA wameonesha kuvutiwa na elimu ya vipimo katika sekta ya mafuta ya petroli, saruji na bidhaa nyingine za ujenzi. Askari wamesema elimu hiyo itawasaidia katika doria za kuhakikisha biashara inafanyika kwa haki, wakati wazee wamesema wamepata uelewa mpya wa kulinda familia zao dhidi ya udanganyifu.

Wananchi wote waliotembelea banda hilo wamepongeza Serikali kwa kuona umuhimu wa kuwa na Wakala wa Vipimo nchini. Wamesema uwepo wa WMA umesaidia kulinda haki za walaji na kuweka mazingira bora ya biashara yanayosadifu kaulimbiu ya maonesho isemayo “Usalama na  Amani ni Kichocheo cha Biashara na Uwekezaji".

 


Wanafunzi kutoka shule mbalimbali za Msingi na Sekondari jijini Mwanza wameomba Wakala wa Vipimo (WMA) kuanzisha Klabu za Vipimo katika shule za Mkoa huo.

Ombi hilo wamelitoa leo Jumamosi, Agosti 29, 2026 walipotembelea banda la WMA katika Maonesho ya Biashara ya Afrika Mashariki yanayoendelea viwanja vya Furahisha, Jijini Mwanza.

Ili kuthibitisha kiu yao ya elimu ya vipimo, mwanafunzi mmoja kutoka Shule ya Msingi Ghana, Ibrahim Omary, alijitolea na kupewa fursa ya kutoa elimu ya vipimo kwa wanafunzi wenzake na wananchi waliotembelea banda hilo. Aliifanya kazi hiyo kwa ufasaha mkubwa na kupata pongezi.

Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Ibrahim alisema: 

“Tuliona kwenye vyombo vya habari wanafunzi wenzetu jijini Dodoma ambao wako katika Klabu za Vipimo wakitoa elimu ya vipimo, tukavutiwa sana. Nasi tunaomba WMA waanzishe klabu hizo kwa shule za Mwanza ili nasi tupate elimu hiyo kwa kina.”

Wanafunzi hao wameahidi kuwa mabalozi wa WMA katika jamii zao kwa kuelimisha wenzao, familia na majirani kuhusu umuhimu wa matumizi sahihi ya vipimo. Wengi wao wamesema ndoto yao ni kuwa Maafisa Vipimo.

Akijibu ombi hilo, Meneja Mawasiliano wa WMA, Bi. Veronica Simba amewaahidi wanafunzi hao kuwa Wakala utaanzisha Klabu za Vipimo katika shule za Mkoa wa Mwanza na hatua kwa hatua katika mikoa mingine yote nchini.

“Lengo letu ni kufikisha elimu ya vipimo kwa watoto tangu awali. Kupitia klabu hizi tunajenga kizazi cha wafanyabiashara na watumiaji wanaojali haki na usawa katika biashara,” amesema Bi. Simba.

Wanafunzi na wananchi wengine wameendelea kufurika katika banda la WMA katika siku ya pili ya maonesho hayo. Wamesema wameridhishwa na elimu wanayopata kuhusu umuhimu wa matumizi sahihi ya vipimo.

Maonesho hayo yameanza tarehe 28 Agosti 2026 na yanahitimishwa tarehe 6 Septemba 2026 yakiwa na  kaulimbiu "Usalama na Amani ni Kichocheo cha Biashara na  Uwekezaji hapa Nchini".  

Katika  Maonesho hayo, WMA inatumia kaulimbiu isemayo “Vipimo Sahihi ni Msingi wa Usalama, Amani na  Uwekezaji wa Biashara ”.

 


 Wakala wa Vipimo (WMA) umetakiwa kupanua mpango wa kuanzisha klabu za vipimo shuleni hadi katika shule za sekondari, ili kuongeza wigo wa elimu ya vipimo na kuhakikisha uelewa wa matumizi sahihi ya vipimo unafika hadi ngazi ya kaya.

Wito huo umetolewa na Mhadhiri wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), Patroba Chaulo, ambaye amepongeza WMA kwa kuanzisha klabu hizo katika shule za msingi, akisema matumizi ya wanafunzi kama mabalozi wa elimu ya vipimo ni mkakati wenye tija kubwa kwa jamii.

Amesema mpango huo unatoa fursa ya kutumia mfumo wa elimu wa “mtoto kwa mtoto” (child-to-child), ambapo wanafunzi huweza kufikisha elimu na ujumbe kwa wenzao kwa urahisi zaidi, na hatimaye kuwafikishia wazazi na familia zao.

Kwa mujibu wa Chaulo, njia hiyo inaweza kuwa na ufanisi mkubwa kwa sababu wanafunzi wana nafasi kubwa ya kushirikiana na kuwasiliana na wenzao kwa lugha rahisi na inayoeleweka, jambo linalorahisisha uenezaji wa elimu ya vipimo.

“Mtoto anaweza kumwelewesha mtoto mwenzake kwa urahisi zaidi kuliko mtu mzima anapojaribu kumwelewesha mwanafunzi. Hii inafanya mfumo wa child-to-child kuwa fursa muhimu katika kueneza elimu ya vipimo,” amesema.

Ameeleza kuwa umuhimu wa mpango huo hauishii shuleni pekee, bali unaweza kusaidia elimu ya vipimo kufika hadi ngazi ya kaya, kwa kuwa wanafunzi wanaotoka katika klabu hizo wanaishi katika familia na jamii mbalimbali.

Amesema kupitia wanafunzi hao, WMA inaweza kuwa na mtandao mpana wa mabalozi ambao utasaidia kufikisha ujumbe kuhusu umuhimu wa vipimo sahihi katika maeneo ambayo ni vigumu kwa Wakala kufika moja kwa moja.

“WMA haiwezi kufika katika kila nyumba, lakini wanafunzi hawa wanatoka katika kaya mbalimbali. Hivyo, wanakuwa kiungo muhimu cha kufikisha elimu hii kutoka shuleni hadi katika familia na jamii kwa ujumla,” amesisitiza.

Chaulo amesema elimu hiyo ni muhimu katika kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu matumizi ya vipimo sahihi na vilivyothibitishwa, hususan katika shughuli za kila siku zinazohusisha biashara na miamala mbalimbali.

Amesema jamii yenye uelewa kuhusu vipimo inaweza kutambua umuhimu wa kuhakikisha bidhaa zinapimwa kwa vipimo sahihi na kulinda haki za watumiaji pamoja na wafanyabiashara.

Kwa msingi huo, amependekeza WMA kuendelea kuimarisha klabu hizo katika shule za msingi na kuzitanua hadi shule za sekondari ili kuwafikia vijana wengi zaidi na kujenga kizazi chenye uelewa mpana kuhusu viwango na vipimo.

Ameongeza kuwa uwekezaji katika elimu ya vipimo kupitia shule ni hatua muhimu ya kujenga utamaduni wa matumizi sahihi ya vipimo nchini, huku wanafunzi wakitumiwa kama sehemu ya suluhisho la kufikisha elimu hiyo katika jamii.

Mpango huo pia unatarajiwa kuongeza uelewa wa Watanzania kuhusu umuhimu wa kuwa na viwango na vipimo sahihi na vilivyothibitishwa (standards in measurements) katika maisha ya kila siku, hususan katika shughuli zinazohusisha biashara, ununuzi na uuzaji wa bidhaa.






 


Na WMA - DODOMA.


Wanafunzi wa Klabu ya Vipimo (Vipimo Club) kutoka Shule ya Msingi Mtemi Mazengo ya jijini Dodoma, wamegeuka walimu kwa siku moja baada ya kumpa elimu ya vipimo Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dennis Londo, katika banda la Wakala wa Vipimo (WMA), kwenye Maonesho ya 33 ya Wakulima Nane Nane, Dodoma.

Leo Agosti 7, 2026, Naibu Waziri Londo alishangazwa na ufasaha wa wanafunzi hao walipomweleza umuhimu wa vipimo sahihi, kuandika kwa usahihi vifungashio katika bidhaa zilizofungashwa pamoja na madhara ya lumbesa.

“Nimefurahishwa sana. Watoto hawa ni mabalozi wazuri wa jamii. Uwekezaji wa WMA katika kizazi kijacho unaleta matokeo,” alisema.

Wanafunzi hao walikuwa katika ziara iliyoratibiwa na Wakala wa Vipimo ikiwa ni sehemu ya mpango wa elimu ya vipimo kwa vitendo.

Mkakati wa WMA ni kuwajengea wanafunzi uelewa wa vipimo kwa nadharia na vitendo ambapo leo wanafunzi hao wa Klabu ya Vipimo ndiyo walikuwa wakitoa huduma zote bandani ikiwemo kuelimisha, kuonyesha matumizi ya vipimo mbalimbali na kujibu maswali ya wananchi.

Naibu Waziri Londo ameonesha kufurahishwa na namna wanafunzi hao walivyojengewa uelewa mpana katika masuala ya vipimo na umahiri wao wa kutoa elimu hiyo kwake na kwa wananchi mbalimbali waliotembelea banda.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi wa Wakala wa Vipimo, Francis Olwero amesema WMA imejipanga kikamilifu kuendeleza klabu za vipimo za wanafunzi ili kuwajengea uelewa wa kivipimo na kurahisisha zaidi usambazaji wa elimu ya vipimo kwa taifa zima wao wakiwa kama mabalozi. 

Amesema wanafunzi hao wamedhihirisha kuwa mbinu hiyo ya kuwaandaa wanafunzi kwa kuwapatia elimu ya vipimo ina tija.

Kiongozi wa Vipimo Club kutoka Mtemi Mazengo, Glory Enock ameishukuru WMA kuanzisha klabu hiyo na kuwapa elimu ya vipimo huku akibainisha kuwa ziara yao NaneNane ililenga pia kusaidia kujenga utamaduni wa “Pima kwa Haki, Pata Faida Halali”

 “Tumefundishwa, sasa tunafundisha wazazi na wafanyabiashara kutumia mizani sahihi,” alisema.

Wananchi waliotembelea banda la WMA waliipongeza na kuitaka iendelee kushirikisha shule nyingine kuanzisha Klabu za Vipimo.




Na WMA - DODOMA.


Wajasiriamali wa kikundi cha Hapa Kazi kutoka Shehia ya Mtemani Wingwi, Wilaya ya Micheweni, Mkoa wa Kaskazini Pemba wametembelea banda la Wakala wa Vipimo (WMA) katika Maonesho ya 33 ya Wakulima Nane Nane yanayofanyika Viwanja vya Dkt. John Samwel Malecela, Nzuguni, jijini Dodoma.

Katika ziara hiyo iliyofanyika leo Agosti 6, 2026, wajasiriamali hao wameshukuru kupata elimu kuhusu matumizi sahihi ya vipimo, ufungashaji bora wa bidhaa na mbinu za kuongeza ushindani wa bidhaa zao sokoni.

Mwakilishi wa kikundi hicho, Asha Mwiaka Haji, amesema maonesho hayo yameendelea kuwafungua macho na kuwaongezea uelewa mkubwa kuhusu vigezo vinavyopaswa kuzingatiwa katika biashara ili bidhaa zao ziweze kupenya kwenye masoko.

“Tumefurahi sana kufika banda la WMA maana sisi pia tuna Wakala kama hii Zanzibar. Tumejifunza jinsi ya kutumia mizani, kuweka lebo sahihi na umuhimu wa vipimo katika biashara yetu, elimu ambayo pia tumekuwa tukiipata kupitia Wakala yetu ya Vipimo Zanzibar,” alisema.

Asha ameeleza kuwa kikundi chao kinajishughulisha na usindikaji na uuzaji wa bidhaa mbalimbali zikiwemo mwani, mafuta ya mgando, sabuni za mwani pamoja na dawa za asili.

Aidha, amesema ushiriki wao katika maonesho hayo umewaongezea ujuzi na uelewa zaidi kuhusu matumizi sahihi ya vipimo, mfumo wa alama za mistari (barcodes) na mbinu bora za kufungasha bidhaa.

“Tunawashukuru WMA kwa elimu hii. Tukirudi kwetu, tutaendelea kuwaelimisha pia wajasiriamali wengine ili tuweze kuzalisha bidhaa zenye ubora na zinazokidhi viwango vya soko,” alisema Asha.

Aidha, Asha amewahimiza wajasiriamali wenzake kushirikiana kwa karibu na maafisa wa Serikali katika ngazi ya shehia na wilaya ili kubuni mikakati itakayoongeza thamani ya bidhaa zao na kuchochea ukuaji wa uchumi.

Wakala wa Vipimo (WMA) inafanya kazi kwa ushirikiano mkubwa na Wakala wa Vipimo Zanzibar (ZAWEMA)

 


 Na. WMA- Dodoma

Wakulima, wafugaji, wavuvi, wafanyabiashara na wananchi wameendelea  kutembelea banda la Wakala wa Vipimo (WMA) Katika siku ya tano ya Maonesho ya Nanenane Kitaifa yanayoendelea jijini Dodoma, wakipatiwa elimu kuhusu umuhimu wa matumizi sahihi ya vipimo.

Katika maonesho hayo, wananchi wamekuwa wakipata fursa ya kujifunza namna ya kutumia na kuhakiki vifaa vya vipimo, pamoja na kuelewa madhara yanayotokana na matumizi ya vipimo visivyo sahihi katika biashara za mbegu, pembejeo, maziwa, mazao na bidhaa nyingine.

Wataalamu wa WMA wamekuwa wakitoa elimu kwa vitendo na kujibu maswali ya wananchi kuhusu taratibu za uhakiki wa vipimo, hatua inayolenga kulinda haki za wakulima, wafanyabiashara na walaji.

WMA imesema itaendelea kutoa elimu hiyo bure kwa wananchi katika siku zote za maonesho hayo, ikiwa na lengo la kuhamasisha matumizi ya vipimo sahihi kwa ajili ya kuongeza tija na kuchangia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Kaulimbiu ya maonesho ya Nanenane Kitaifa 2026 ni: "Tambua Soko; Ongeza Tija Kutekeleza Dira 2050"

 


Mkurugenzi wa Sera na Mipango wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Bw. Needpeace Wambuya leo Agosti 2, 2026 ametembelea banda la Wakala wa Vipimo (WMA) katika Maonesho ya Wakulima, Mifugo na Uvuvi (Nane Nane) yanayofanyika Viwanja vya Dkt. John Samuel Malecela Nzuguni jijini Dodoma.

Katika ziara hiyo aliyomwakilisha Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga, Mkurugenzi Wambuya alipongeza juhudi za WMA za kutoa elimu kwa wakulima, wafugaji na wajasiriamali kuhusu umuhimu wa vipimo sahihi. Hata hivyo aliwataka watumishi kuongeza bidii, juhudi na maarifa katika utoaji wa huduma ili kuhakikisha huduma za uhakiki wa vipimo zinafikia wadau wote wa sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi.

 “Kazi yenu ni muhimu katika kulinda haki za wazalishaji na walaji. Niwahimize muendelee na kasi hii kwa kutumia teknolojia ili kila mkulima na mfanyabiashara apate uelewa na kushawishika kutumia vipimo sahihi” alisema.

Pia Mkurugenzi Wambuya alitoa wito kwa Wakala kuharakisha michakato ya utekelezaji wa huduma mpya za kivipimo zilizopangwa na Serikali ili zianze kutoa manufaa kwa wananchi mara moja. 

Alisisitiza kuwa Serikali imeweka nguvu katika kuboresha sekta ya vipimo ili kuongeza tija na ushindani wa bidhaa za Kitanzania sokoni ndani na nje ya nchi.

 


Wakala wa Vipimo (WMA) umeanza kutoa elimu ya vipimo kwa wakulima, wafugaji na wavuvi katika siku ya kwanza, (Agosti 1, 2026) ya Maonesho ya Wakulima Nane Nane yanayofanyika kitaifa katika Viwanja vya John Malecela, eneo la Nzuguni jijini Dodoma.

Kwenye banda lake lenye kaulimbiu 

"Usahihi wa Vipimo vya Mbegu, Pembejeo, Mazao  na Bidhaa Sokoni ni Msingi wa Tija na Utekelezaji wa Dira 2050," Maafisa Vipimo wa WMA wanatoa elimu ya vipimo na majukumu ya Wakala kwa ujumla katika kulinda haki za wakulima, wafugaji, wavuvi na wanunuzi.  

Akizungumza na waandishi wa habari, Meneja Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma wa WMA Bi. Veronica Simba alisema lengo ni kuhakikisha kila mkulima, mfugaji na mvuvi anaelewa umuhimu wa kutumia mizani na vipimo vingine vilivyohakikiwa na WMA. 

“Kama unauza mahindi, mbolea au maziwa, na kama unanunua pembejeo za mifugo au samaki, kipimo sahihi ndiyo msingi wa faida. Tunataka kila mtu atoke hapa Nane Nane akiwa na uelewa wa kutambua na kudai kipimo sahihi,” alisisitiza Bi. Veronica.

Bi. Veronica aliwataka wakulima, wafugaji, wavuvi na wananchi kwa ujumla kutembelea banda la WMA katika kipindi chote cha maonesho hayo. “Wataalamu wetu wapo hapa kutoa elimu bure. Njoo ujifunze, uulize maswali na hata kutoa maoni yako,” aliongeza.

WMA imesema itatumia kipindi chote cha maonesho hayo kuhamasisha matumizi ya vipimo sahihi kama njia moja ya kutekeleza Kauli Mbiu ya Taifa ya  NaneNane 2026 "Tambua Soko, Ongeza Tija, Kutekeleza Dira 2050" na kuhakikisha sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi inakuwa na ushindani na uhakika wa soko.







 


Katika siku ya nane (08) ya Maonesho ya Biashara ya Kimataifa maarufu kama SabaSaba, yanayoendelea jijini Dar es Salaam, Wakala wa Vipimo (WMA) imeendeleza mkakati wake wa kuwatembelea wajasiriamali na kuwapatia elimu kuhusu matumizi sahihi ya vipimo. 

Zoezi la utoaji elimu ya vipimo kwa wajasiriamali linaenda sambamba na kuhudumia wadau mbalimbali wanaotembelea banda la WMA katika Maonesho hayo ya SabaSaba. 

Lengo ni kuhakikisha elimu na huduma mbalimbali za ki-vipimo zinafikishwa kwa wadau wengi kadri iwezekanavyo.

Pichani ni matukio mbalimbali kuhusu utoaji elimu na huduma za ki-vipimo kwa wananchi na wadau, leo Julai 05, 2026.





 

 Katika siku ya tano ya Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa (SabaSaba), Julai 2, 2026, Maafisa kutoka Wakala wa Vipimo (WMA) wamewatembelea wajasiriamali mbalimbali na kuwapatia elimu ya vipimo.

Wakiongozwa na Meneja wa WMA Mkoa wa Ki-vipimo Ilala, Bw. Muhono Nashon, wataalamu hao wa vipimo wamewaelimisha wajasiariamali wadogo wadogo namna sahihi ya uandishi wa alama katika vifungashio vya bidhaa zao ili zikidhi vigezo vya soko la kimataifa, pamoja na masuala mengine muhimu kuhusu vipimo.

Akizungumzia hatua hiyo, Meneja Mawasiliano wa WMA, Bi Veronica Simba amesema ni mojawapo ya mbinu za kuwafikia wadau mbalimbali wa vipimo wanaoshiriki katika Maonesho hayo.

Aidha, ameongeza kuwa, hatua hiyo pia imelenga kutekeleza maelekezo ya Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga ambaye awali alipotembelea Banda la Wizara pamoja na Taasisi zake, aliwataka watumishi hao kuwafuata wadau mbalimbali na kuwapatia huduma badala ya kusubiri wale tu wanaofika bandani.

Utaratibu huo umepongezwa na wajasiriamali waliofikiwa wakisema kuwa umewawezesha kupata elimu ya vipimo pasipo kulazimika kuacha mabanda yao kwenda katika banda la WMA kufuata huduma hiyo.

Utoaji elimu ya vipimo kwa wadau mbalimbali ni utaratibu wa kawaida ambao hutekelezwa siku zote na WMA kama sehemu ya majukumu ya kazi.





 


“Sasa najua ni nini ninapaswa kuangalia ninapojaza mafuta, kununua sukari au hata ninaponunua gesi ya kupikia.” Ni kauli ya Bw. Bilson Vedastus, mmoja wa wananchi waliotembelea banda la Wakala wa Vipimo (WMA) katika Maonesho ya Kitaifa ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea Viwanja vya Chinangali Park, Dodoma.

Banda hilo limekuwa kitovu cha msongamano siku ya tatu ya maonesho, Juni 18, 2026 huku wananchi wakijitokeza kwa wingi kujifunza jinsi Serikali kupitia WMA inavyohakikisha kila kipimo kinachotumika kibiashara na katika huduma ni sahihi. Maonesho yalianza tarehe 16 Juni na yanatarajiwa kuhitimishwa tarehe 23 Juni 2026.

Baada ya kupata maelezo ya hatua kwa hatua kutoka kwa wataalamu, wengi wameahidi kuwa mabalozi wa Wakala wa Vipimo katika maeneo yao. 

“Tumeona jinsi pampu, mizani na vifaa vingine vinavyohakikiwa kuhakikisha vinapima kwa usahihi. Sasa hatuwezi kukaa kimya tukiona mteja anadhulumiwa. Tutawaeleza jirani zetu na kuripoti udanganyifu popote tutakapouona,” alisema Bi. Asha Siyaya.

Wataalamu wa WMA, Albogast Kajungu, Mbwana Amani na Said Ibrahim waliwaeleza wananchi kuwa uhakiki wa vipimo unagusa sekta zote zinazowahusu moja kwa moja kila siku. Katika sekta ya mafuta, pampu zote huhakikiwa na kuwekewa stika ya uthibitisho. Sokoni na madukani, mizani inayotumika kupimia sukari, mchele na mboga hufanyiwa ukaguzi ili mteja asipoteze pesa.

Sekta ya maji na umeme nayo haikuachwa nyuma. Mita za maji na umeme zinazotumika nyumbani na kwenye biashara ndogo huhakikiwa na kuthibitishwa ili kuhakikisha mteja analipia matumizi halisi na si makadirio au idadi isiyo sahihi. Vile vile mitungi ya gesi ya kupikia, bidhaa zilizofungashwa kama unga na sabuni, pamoja na mizani za barabarani zote huhakikiwa mara kwa mara.

Akizungumza na Waandishi wa Habari, Meneja Mawasiliano wa Wakala wa Vipimo, Bi Veronica Simba amesema lengo ni moja: kuhakikisha mwananchi anapata thamani kamili ya kila shilingi anayolipa, na amewahamasisha wananchi wengi zaidi kutembelea banda hilo kabla ya maonesho kuhitimishwa.






 


Wadau mbalimbali waliotembelea Banda la Wakala wa Vipimo (WMA) katika siku ya kwanza ya Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma, Juni 16, 2026 wamekiri kuvutiwa na elimu inayotolewa na timu ya wataalamu kuhusu matumizi sahihi ya vipimo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Nadhifa Nyoni kutoka Mamlaka ya Maji (TANGA UWASA), Rose Mmary (JWTZ) na Janeth Matara, mwananchi mkazi wa Dodoma, wamepongeza kazi zinazofanywa na WMA na kukiri kuwa elimu waliyoipata kutoka kwa wataalamu imewaongezea uelewa kuhusu vipimo.

Kwa upande wake, Abbas Kayanda, mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma, pamoja na kupongeza kazi nzuri inayofanywa na WMA, ameshauri kuongeza nguvu katika utoaji elimu ya vipimo ili kuwapatia uelewa wananchi wengi zaidi hususan walioko vijijini.

Ufunguzi rasmi wa Maadhimisho ya Kitaifa ya Wiki ya Utumishi wa Umma kwa mwaka 2026 yaliyoanza leo, Juni 16 katika uwanja wa Chinangali Dodoma, yatahitimishwa Juni 23.

Kaulimbiu ya mwaka huu ni "Kuchochea Uwajibikaji Jumuishi kwa Maendeleo Endelevu."