Kuelekea siku ya Utalii Duniani Septemba 27, 2025 Chuo Cha Uhasibu Arusha-IAA kimeandaa kongamano la kimataifa la utalii Arusha 2025 kuwakutanisha wadau wa utalii kujadili mustakabali mzima wa sekta ya utalii.

Kongamano hilo lenye kauli mbiu "Utalii na maendeleo endelevu" limefanyika leo 24 Septemba, 2025 katika Ukumbi wa Gran Melia Arusha; ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) eneo la ushirikishwaji wadau kwa lengo la kupata ushauri wa kisekta katika kuboresha sekta ya utalii.

Akizungumza wakati wa ufunguzi Mkuu wa Chuo IAA Prof. Eliamani Sedoyeka amesema, lengo la kongamano ni kutoa nafasi ya kujadiliana, kuibua mawazo mbalimbali na kupata mrejesho kutoka kwa wadau wa utalii utakaoleta tija ya maendeleo endelevu katika sekta ya utalii na kuendana na mabadiliko yanayotokea.

"Sisi kama Chuo kupitia kongamano hili tunapata mrejesho wa nini mategemeo ya sekta, hiyo inapelekea sisi kujipanga vizuri kwenye kutoa wataalamu ambao wanaendana na mategemeo na muelekeo wa sekta" Amesema Prof Sedoyeka.

Aidha, Prof. Sedoyeka ameongeza kuwa IAA ni wadau wakubwa sana wa utalii kwa vitendo kupitia utoaji wa fani ya Utalii na Ukarimu ambayo inatoa wahitimu wenye ubobevu na umahiri mkubwa kuweza kuleta maendeleo katika utalii. 

Pia, amesisitiza umuhimu wa kufanya shughuli za utalii bila kuleta madhara ya kimazingira au kiutamaduni katika maeneo ya kiutalii kwa faida ya kizazi cha sasa na kijacho.

Kwa upande wao wadau wa utalii akiwemo Ms Caudence Ayoti na Dkt. Charles Raphael wamesema ni kongamano muhimu litakalowezesha maendeleo ya utalii nchini, kwani limetoa nafasi ya kuwasilisha tafiti mbalimbali walizofanya hususani katika teknolojia ya utalii na mabadiliko yake.















Share To:

Post A Comment: