Na Oscar Assenga,TANGA

MWENGE wa Uhuru unatarajiwa kuwasili katika wilaya ya Tanga Jumatatu June 16 mwaka huu na upitia katika miradi saba ya maendeleo yenye thamani ya Sh.Bilioni 3,058,289,671.99.

Akizungumza na waandishi wa habari wakati akitoa taarifa za ujio wa Mwenge huo,Mkuu wa wilaya ya Tanga Dadi H.Kolimba alisema wataupokea ukitokea wilayani Mkinga katika uwanja wa shule ya Msingi Mabambani Mtaa wa Mpirani Kata ya Chongoleani.

Aliitaja miradi ambayo itapitiwa na Mwenge ni ujenzi wa madarasa 4 ya Ghorofa ,matundu 13 ya vyoo na ofisi, shule ya Msingi Mbuyuni yenye thamani ya sh. 388,769,596.80/= na Ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa ya awali ya mfano shule ya msingi Mwakidila yenye thamani ya sh. 70,100,000.00.

Mkuu huyo aliitaja miradi mingine kuwa ni ujenzi wa ofisi ya mtendaji kata ya Tongoni uliogharimu kiasi cha sh. 85,000,000.00, ujenzi wa barabara ya Sahare awamu ya kwanza na ya pili yenye urefu wa mita 600 kwa kiwango cha lami  Kwa thamani ya Sh 489,606,700/00.

“Lakini pia Mwenge utapita katika ujenzi wa Jengo la X-Ray kituo cha Afya Makorora wenye thamani ya Sh. 84,721,640/00 pamoja na mradi wa ufungaji wa dira za maji za malipo ya kabla awamu ya kwanza wenye thamani ya Sh. 1,872,091,735.00 “Alisema 
 
Hata hivyo alisema kwamba mradi mwingine ambao utapitiwa na mwenge ni mradi wa kikundi cha vijana cha kutengeneza gypsum wenye thamani ya Sh.68,000,000/-

Alisema mbali na miradi hiyo saba mwenge wa uhuru utakagua shughuli za maandalizi ya uchaguzi,  kongamano la vijana pamoja na maswala mtambuka.

Mwisho.
Share To:

OSCAR ASSENGA

Post A Comment: