Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba (Mb), ameshuhudia tukio la kumtunuku Dkt. Akinwumi Adesina, Rais anayeondoka wa Benki ya Maendeleo ya Afrika, Shahada ya Heshima ya Uzamivu (Honoris Causa), iliyotolewa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam jana tarehe 13 Juni 2025, kwa kutambua mchango wake mkubwa katika maendeleo ya Afrika katika zama za sasa.
Mhe. Dkt. Nchemba alisema kuwa heshima hiyo ni uthibitisho wa yale ambayo wengi barani Afrika na duniani wanayajua tayari kwamba Dkt. Adesina ni kiongozi mwenye maono, bingwa wa maendeleo, na mwana wa kweli wa Afrika aliyejitolea kubadili simulizi la bara hili na kwamba Tanzania inajivunia kuwa miongoni mwa mataifa yanayosherehekea mafanikio na urithi wake wa kipekee.
Alisema kuwa kupitia mpango wa Building a Better Tomorrow (BBT), Vijana katika Kilimo Biashara, Benki ya Maendeleo ya Afrika chini ya uongozi wa Dkt. Adesina imewezesha zaidi ya vijana 11,000 wa Kitanzania kuwa wajasiriamali wa kilimo. Kwa kuwapatia ardhi, pembejeo, na mikopo, mpango huu haukuwa tu ajira kwa vijana bali umeleta matumaini mapya vijijini kuwa ustawi unawezekana.
“Dhamira ya Dkt. Adesina kwa Tanzania pia ilidhihirika wakati wa janga la COVID-19, moja ya nyakati ngumu zaidi kwa dunia nzima, Chini ya uongozi wake, Benki ilitoa msaada wa kifedha wa takribani dola za Marekani milioni 50, uliosaidia serikali yetu kushughulikia dharura ya afya, kuendeleza uchumi, na kuwalinda wanyonge” alisema Mhe. Dkt. Nchemba
Alieleza kuwa athari za Dkt. Adesina hazikuishia Tanzania pekee bali aliongoza ajenda mpya ya maendeleo Afrika. Pamoja na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Benki ya Dunia, Bw. Ajay Banga, aliasisi Mkutano wa Nishati Afrika na kuanzisha Mission 300, lengo la kuhakikisha upatikanaji wa nishati kwa Waafrika milioni 300 ifikapo mwaka 2030.
“Katika majukwaa ya kimataifa, Dkt. Adesina amekuwa sauti ya kuaminika ya Afrika, akitetea upatikanaji wa fedha kwa mabadiliko ya tabianchi, usalama wa chakula, na usawa katika ushirikiano wa kiuchumi unaozingatia matarajio ya mataifa ya Afrika” alisisitiza Dkt. Nchemba
Alisema kuwa chini ya uongozi wake, Benki ya Maendeleo ya Afrika ilileta mtazamo mpya wa kugharamia miradi mikubwa yenye athari za moja kwa moja. Kinyume na mikopo ya awali iliyokuwa ikigusa maeneo mengi bila athari kubwa kwa watu, ambapo Dkt. Adesina alihakikisha miradi yenye tija inapata msukumo.
Dkt. Nchemba alitaja baadhi ya miradi inayofadhiliwa na AfDB hapa nchini kuwa ni pamoja na
Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato, Dodoma
Barabara ya Iringa – Dodoma – Babati
Barabara ya mzunguko wa mji wa Dodoma
Mradi wa Maji safi na Usafi wa Mazingira (AUWSA – Arusha) uliowafikia zaidi ya wakazi 600,000 wa Arusha na Viunga vyake.
Katika sekta ya nishati, kuna miradi kadhaa ikiwemo Mradi wa Gridi ya Kaskazini Magharibi – (msongo wa kilovolti 400 kutoka Nyakanazi hadi Kigoma), ambao umeongeza uwezo wa gridi ya taifa katika mikoa ya Kigoma na Kagera.
Na zaidi ya yote, usaidizi katika reli ya SGR – Lot 6 (Tabora–Kigoma), na Lot 7 (Uvinza–Musongati, Burundi hadi DRC).
“Dkt. Adesina, urithi wako unaacha funzo kwa taasisi zote za kimataifa – kuwa msaada kwa Afrika lazima uambatane na mipango ya kitaifa, usiwe wa masharti yasiyokubalika, na uzingatie miradi ya kimkakati yenye uwezo wa kubadilisha maisha ya watu. Sio mikopo ya “chapati na mandazi” inayoongeza madeni bila kuleta mabadiliko” aliongeza Dkt. Nchemba
Alisema kuwa ni jambo la heshima kubwa kuona Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, taasisi ya elimu ya juu ya muda mrefu na inayoheshimika sana, kumtunuku shahada hiyo ya heshima ambayo ni ishara ya heshima ya kitaaluma, na shukrani kwa ubora, mshikamano wa Kiafrika, na uongozi wa kweli.
Alitumia pia fursa hiyo kumpongeza kwa dhati Rais mpya Mteule wa Benki ya Maendeleo ya Afrika, Raia wa Mauritania, Dkt. Sidi Ould Tah kwa kuchaguliwa Tarehe 29 Mei 2025, kuiongoza Benki hiyo kuanzia mwezi Septemba 2025 na kumtakia mafanikio makubwa katika nafasi hiyo muhimu.
Post A Comment: