Na, Egidia Vedasto, Msumba News
Wananchi Jijini Arusha wametakiwa kuepuka kutupa taka ovyo hususan chupa za plastiki, na atakayefanya hivyo kukiona cha moto kwa kulipa faini ya papo hapo isiyopungua shilingi 50,000/=.
Amezungumza hayo wakati wa uzinduzi wa wa maadhimisho ya siku mazingira Duniani uliofanyika Stendi kubwa ya mabasi Jijini Arusha, Katibu tawala wa Wilaya ya Arusha Jacob Julius Rombo amesisitiza sheria ndogo zilizowekwa kuhusu mazingira kutumika ili kila mmoja awajibike pale atakapobainika akifanya uchafuzi wa holela.
Amewataka Watendaji wa Kata na Mitaa kusimamia vyema sheria hizo, katika maeneo yao na mahali wananchi wanapofanyia biashara ili kuhakikisha utamaduni wa usafi wamazingira unaendelezwa.
"Sheria zipo lakini nafikiri hazitumiki sawasawa kuwabana wanaochafua mazingira, naamini kama wangeguswa na faini hizo tungeona mabadiliko, sasa umefika wakati sahihi wa kuzitumia vizuri sheria hizi ili watakaobainika walipe faini, nafikiri watakuwa mabalozi kwa wengine na si hivyo tu bali watasaidia kuongeza mapato yetu" amesema Rombo.
Hata hivyo amewapongeza Vijana wa Jeshi la Akiba, Wakuu wa Idara na Watumishi mbalimbali kwa kushirikiana na Wananchi wa maeneo ya Soko kuu na Stendi kuu ya mabasi waliojitokeza kushiriki zoezi la usafi kuelekea siku ya mazingira Duniani.
Kwa upande wake mkuu wa kitengo cha udhibiti wa taka na usafi wa mazingira James Lobikoki amesema kila mmoja awajibike kufanya usafi katika eneno lake na kupunguza matumizi ya plastiki.
"Nawakumbusha wananchi kuwa usafi unaanza na mtu mwenyewe, tujipende na tupende mazingira yanayotuzunguka ili kufanya Jiji letu kuwa safi" amesema Lobikoki.
Vile vile Diwani wa Kata ya Ngarenaro Doita Isaya akimwakilisha Meya wa Jiji la Arusha Maxmillian Iranqhe amesema kwa kushirikiana na viongozi mbalimbali wa mitaa atahakikisha zoezi hilo linakuwa endelevu.
"Nimeshangazwa na baadhi ya wananchi waliokuwa wakiwashangaa wenzao wakiendelea na usafi, ifahamike kuwa usafi ni wajibu wa kila mmoja katika eneo lake, hivyo naamini haitaishia hapa bali itakuwa mwendelezo wa kilichofanyika leo" amesema Doita.
Katika namna hiyohiyo Mjasiriamali katika eneo la stendi kuu ya mabasi Rabia Hamis amekiri kuwepo tofauti baada kufanyikq usafi katika eneo hio.
" Kwa kweli leo mazingira yamekuwa safi, yanavutia, nawashauri wenzangu wanaofanya biashara katika eneo hili tufanyie usafi maeneo yetu ili kuepuka faini itakayotutaka kutoa 50000 pale tutakapokutwa na makosa"amesema Rabia.
Kilele cha maadhimisho ya siku ya mazingira Duniani kinatarajiwa kufanyika Juni 05 2025 nchini Korea Kidunia, na Jijini Dodoma kwa hapa Tanzania ikibeba kaulimbiu "Mazingira yetu Tanzania ijayo Tiwajibike sasa, Dhibiti Matumizi ya Plastiki".
Post A Comment: