Na, Egidia Vedasto, Msumba News 

Shrika la Okoa New Generation kwa kushirikiana na Restless Development wametoa elimu ya kodi kwa vijana takriban 30 Jijini  Arusha  . 

Shirika limekuwa na desturi ya kutoa elimu hiyo kupitia mradi wa  "Kijana Wajibika, Shiriki Lipa Kodi" kwa vijana wabunifu, wajasiriamali na wenye mpango kuanzisha biashara ili waweze kupata maarifa na nini wafanye kabla na baada ya kuanzisha biashara.

Shirika hilo limewalenga vijana kwa kuwa ndio nguvu kazi ya taifa, na kwa mujibu wa takwimu ya sensa ya mwaka 2022 inaonyesha vijana kuwa ndio kundi kubwa lenye idadi ya watu asilimia 34.5 ya watanzania wote, hali inayoleta ushawishi katika mchakato wowote wa maendeleo ya taifa. 

Kwa upande wake Mratibu wa Mradi wa Kijana Wajibika Shiriki Lipa Kodi Shaban James  amesema lengo la mradi ni kuona vijana wengi wanapata uelewa na kuwa wazalendo katika suala la kulipa kodi na kuongeza pato la taifa. 

Ameongeza kuwa kulipa kodi ni jukumu la kila kijana aliyefikisha umri wa miaka 18, hivyo ni muhimu kuijua vizuri kodi kwa maana nani alipe na kwa wakati gani badala ya kukwepa na kujenga chuki kila ikitajwa kodi. 

"Vijana wengi wamepata mwanga na majibu ya maswali waliyokuwa nayo juu ya kodi, ombi langu kwa viongozi wa serikali na mamlaka ya mapato nchini TRA ni kuendelea kushirikiana na makundi ya vijana kuwapa elimu  juu ya kodi na fulsa zitakazowasaidia kuinua uchumi wao" amesema Shaban. 

Afisa mwandamizi TRA Nicodemus Massawe ambaye ametoa elimu  ya kodi kwa vijana hao, amepongeza uelewa na utayari walionao vijana katika masuala ya kodi. 

Amewataka kutokatishwa tamaa na baadhi ya watu wachache wanaochukulia kodi kama ukatili, bali kupata elimu na ushauri kutoka sehemu sahihi, Ofisi za mamlaka ya mapato nchini TRA na Watumishi wake.

"Kupitia mafunzo haya nimewapa elimu juu ya bidhaa ambazo hazitozwi kodi, faida za matumizi ya mashine ya kutolea risiti (EFDs) kusajiri biashara zao, namna ya kupata namba ya utambulisho wa biashara(TIN) na kulipa kodi kwa uaminifu" amesema Massawe. 

Katika namna hiyohiyo Mwezeshaji wa usawa wa kodi Ibrahim Abdallah amesema kuwa ni muhimu vijana kufahamu sera za usawa wa kodi ili kuhakikisha nchi inapata mapato ya kujenga miradi. 

"Kupitia mafunzo haya tumeunga kikundi kazi kitakachoboresha sera hizo kwa hapa Arusha na nchi nzima, ili kila Mtanzania ajue kuwa kudai risiti ni wajibu wake sio hiari" amefafanua Ibrahim. 

Vilevile Afisa maendeleo ya vijana na sekretarieti ya mkoa wa Arusha Japheth Majura amewakumbusha Maafisa vijana kukutana na vikundi vya vijana kujua changamoto zao na kuwasaidia kuibua fulsa zilizopo katika halmashauri ili waweze kufikia malengo yao na kumiliki uchumi mzuri. 

"Ikumbukwe nchi yoyote ili iendelee lazima watu wake walipe kodi, naamini vijana wakielimika taifa limeelimika, hivyo mkaizingatie elimu hii ili iwafae katika maisha yenu" amesema Majura. 

Mmoja wa washiriki wa mafunzo ya kodi Regina Mkanda Mbunifu na Mwananfunzi wa chuo cha Ufundi Arusha, ameshukuru kupata mafunzo hayo yaliyomaliza kiu ya maswali aliyokuwa nayo juu ya masuala ya kodi. 

"Awali mimi nilikuwa miongoni mwa wale wasiotaka kusikia kuhusu kodi, na sasa nimefahamu kuwa ni jukumu la lazima kwa kila Mtanzania mwenye umri 18 kulipa kodi ili serikali iweze kutuhudumia" amesema Regina. 



Share To:

Post A Comment: