Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), amelihakikishia Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) kwamba, Serikali itaendelea kufanya maboresho ya sera na mipango yake kwa kuhakikisha sekta mbalimbali za kiuchumi na kijamii zikiwemo sekta za elimu na afya zinapewa kipaumbele katika Bajeti ya Serikali.

Dkt. Nchemba amesema hayo wakati akifunga vikao vya majadiliano kati ya Serikali na Timu ya Wataalam kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), baada ya kukamilisha tathimini ya awamu ya tatu ya utekelezaji wa program ya Extended Credit Facility-(ECF), inayohusisha upatikanaji wa mkopo nafuu kwa ajili ya kuimarisha uchumi wa nchi kupitia sekta za uzalishaji na huduma za jamii pamoja na maombi mapya ya Serikali ya kupata fedha za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kupitia dirisha la Resilient and Sustainable Fund (RSF) kutoka Shirika hilo.

Akifunga vikao hivyo katika Kikao cha majumuisho kilichofanyika kwa njia ya mtandao akiwa Benki Kuu  ya Tanzania Tawi la Arusha huku ujumbe wa IMF na timu ya wataalamu wa serikali wakiwa Benki Kuu ya Tanzania, jijini Dar es Salaam, Dkt. Nchemba, alieleza kufurahishwa kwake na taarifa ya awali iliyowasilishwa na Kiongozi wa Timu hiyo Bw. Harris Charalambos Tsangarides, inayoonesha kuwa Tanzania imetekeleza ipasavyo vigezo vilivyowekwa na Shirika hilo katika mpango huo wa ECF.

Dkt. Nchemba alisema kuwa Serikali itaendelea kutoa kipaumbele katika  Bajeti kwa Sekta ya Elimu kwa kuwa Serikali imefanya maboresho makubwa ikiwemo kuboreshwa kwa mitaala ya elimu pamoja na umuhimu wa kujenga miundombinu itakayo wezesha utoaji elimu inayokidhi mahitaji ya kukuza ajira na ujuzi hususan kwa vijana.

Alisema kuwa Sekta ya Afya pia  itaendelea kupewa kipaumbele kwa kuwa ni sekta muhimu hususan katika kipindi hiki ambapo Bunge limepitisha Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote yenye lengo la kuimarisha huduma za afya kwa Watoto, mama wajawazito pamoja na wazee ili kujenga Taifa imara kiafya.

Aliahidi kuwa Serikali itaendelea kusimamia ipasavyo program hiyo yenye thamani ya dola za Kimarekani bilioni 1.1 ambazo ni sawa na shilingi trilioni 2.4, ambayo itatekelezwa katika kipindi cha miaka minne kuanzaia mwaka 2022/2023 hadi mwaka 2025/2026.

Kuhusiana na maombi ya mkopo mpya kupitia dirisha la RSF kwa ajili ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, Dkt. Nchemba alieleza kuwa Serikali imejipanga kikamilifu kutekeleza hatua za kisera (Reform Measures) zilizobainishwa, kwa vile maboresho hayo yana manufaa makubwa kwa taifa letu.

Kwa upande wake, Bw. Harris Charalambos Tsangarides, alisema kuwa tathimini yao ya awamu ya tatu imeonesha kuwa Tanzania imetekeleza vizuri mpango wa ECF na kushauri hatua kadhaa zinazotakiwa kuendelea kuchukuliwa ikiwemo kuimarisha zaidi huduma za jamii, kusimamia kikamilifu soko la fedha za kigeni, kuongeza ukusanyaji wa mapato ya ndani  pamoja na kuchukua hatua madhubuti za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Alisema kuwa mapendekezo ya tathimini hiyo yatapelekwa mbele ya Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na kwamba uamuzi utakaotolewa na Bodi hiyo utatolewa taarifa kwa umma. 

Tanzania imefanyiwa Tathimini ya Awamu ya Tatu ili iweze kupata fedha kutoka IMF kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya kiuchumi na kijamii ambapo hadi sasa imepokea kiasi cha dola za Marekani milioni 455.3 kati ya dola za Marekani bilioni 1.1 ambazo Tanzania itanufaika nazo katika kipindi cha utekelezaji wa program ya ECF. Aidha, iwapo mapendekezo ya Serikali ya programı mpya ya RSF yataridhiwa na Bodi ya IMF, Tanzania itaongezewa fedha za mkopo nafuu ambazo zitatolewa kwa kıpindi cha miaka miwili (2025/2026).

Share To:

Post A Comment: