Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Christian Makonda amemuomba Mhe. Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi kuiunganisha Zanzibar na Mkoa wa Arusha kwenye sekta ya utalii ili kuwezesha mabadilishano ya Watalii wa pande hizo mbili.

Mhe. Paul Christian Makonda pia amemuomba Mhe. Rais wa Zanzibar Dkt. Hussein Ali Mwinyi kutangaza fursa na vivutio vya Uwekezaji vilivyopo Mkoani Arusha katika adhma ya kutimiza maelekezo ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuongeza vyumba na Vitanda vya kulala wageni mkoani Arusha.

Mkuu wa Mkoa wa Arusha ametoa maombi hayo leo Mei 17, 2024 mbele ya Rais wa Zanzibar Dkt. Hussein Ali Mwinyi akiwa ndiye mgeni rasmi kwenye Semina maalum ya wanahisa wa Benki ya CRDB, semina inayofanyika kwenye Kituo cha kimataifa cha Mikutano mjini Arusha - AICC.

Katika hatua nyingine Mhe. Mkuu wa mkoa ameishukuru benki ya CRDB kwa kuwa mdau mkubwa wa maendeleo ya Mkoa wa Arusha pamoja na kuichagua Arusha kuwa Mwenyeji wa semina na mikutano yao Mikuu suala linalowanufaisha wafanyabiashara na wananchi mbalimbali wa Mkoa wa Arusha.

Katika majibu yake Mhe. Rais wa Zanzibar Dkt. Hussein Ali Mwinyi amemuahidi Mhe. Mkuu wa Mkoa kuwa atatetekeleza maombi yake ipasavyo hasa katika suala la uwekezaji wa ujenzi wa hoteli na nyumba za kulala wageni kutokana na idadi kubwa ya Wawekezaji wanaofika Zanzibar kutaka kuwekeza kwenye ujenzi wa nyumba na vyumba vya kulala wageni na watalii wanaofika nchini.

Akiapishwa mwishoni mwa Mwezi Machi Mwaka Huu, Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan alimuagiza Mkuu wa mkoa wa kukuza utalii wa Arusha pamoja na kuongeza idadi ya vyumba na vitanda vya kulala wageni na watalii kutokana na upungufu mkubwa unaotokana na matokeo chanya ya filamu ya 'The Royal Tour Tanzania' iliyokuwa na nia ya kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo nchini Tanzania ikiwemo vile vilivyopo mkoani Arusha kilipo kitovu cha Utalii Kaskazini mwa Tanzania.

Share To:

Post A Comment: