Mkoa wa Rukwa umejidhihirisha kwa kasi kama kitovu kipya cha kimataifa cha biashara ya madini, hatua inayojengwa na utajiri mkubwa wa rasilimali, miundombinu bora, usalama ulioboreshwa na mifumo rafiki ya Serikali katika usimamizi wa sekta hiyo. Hali hii imeufanya Mkoa huo kuwa miongoni mwa maeneo yanayoongoza kwa kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.
Akizungumza Desemba 04, 2025, Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Rukwa, Mhandisi Joseph Kumburu, amesema Serikali imeweka mazingira madhubuti ya kuongeza uwekezaji kupitia mabadiliko makubwa katika utoaji wa leseni, usimamizi wa masoko ya madini na kuimarisha miundombinu ya kusafirisha bidhaa ndani na nje ya nchi.
Amesisitiza kuwa Rukwa sasa inatambulika kimataifa kutokana na aina mbalimbali za madini pamoja na hatua za Serikali kuimarisha utawala bora na kupunguza urasimu katika mchakato mzima wa uwekezaji.
Kwa mujibu wa Mhandisi Kumburu, zaidi ya leseni 480 za madini tayari zimetolewa katika Mkoa wa Rukwa na maombi mengine zaidi ya 600 yanaendelea kushughulikiwa kupitia mifumo ya kidigitali ya Tume ya Madini, hatua iliyoongeza uwazi na kasi ya utoaji wa leseni. Takwimu zinaonesha kwamba kwa mwaka wa fedha 2024/2025, jumla ya tani 337.6 za madini mbalimbali ziliuzwa katika masoko na vituo rasmi vya Rukwa, zenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 264, huku Serikali ikikusanya zaidi ya shilingi milioni 18 kupitia mrabaha, ada za ukaguzi na vibali vya usafirishaji.
Aidha, Ofisi ilikusanya jumla ya kiasi cha shilingi milioni 656.2 sawa na asilimia 87.5 ya makusanyo yote kwa mwaka wa fedha 2024/2025.
Rukwa inajivunia aina nyingi za madini ikiwemo dhahabu, shaba, makaa ya mawe, madini ya viwandani, vito na madini ya kimkakati kama helium na rare earth elements. Aidha, kijiografia Mkoa una faida ya pekee kutokana na kupakana na Zambia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), pamoja na kuwa na Bandari ya Ziwa Tanganyika inayorahisisha biashara ya kimataifa na usafirishaji wa vifaa vya uchimbaji.
Kwa upande wa wachimbaji wadogo, Serikali inaendelea kutenga na kupima zaidi ya hekta 13,000 zitakazotumika kuendeleza shughuli za uchimbaji mdogo, ambapo maeneo hayo yanatarajiwa kutoa zaidi ya leseni 700. Mahitaji makubwa ya vifaa vya ujenzi kutokana na miradi ya kimkakati pia yamefungua milango kwa wawekezaji kuanzisha mitambo ya kuzalisha mazao kama kokoto, mchanga, kifusi na mawe.
Mhandisi Kumburu amesema mpango wa Mkoa unalenga kuimarisha masoko ya madini, kupanua masoko mapya ndani na nje ya nchi, kuwaunganisha wachimbaji na taasisi za kifedha pamoja na kuongeza ulinzi na matumizi ya teknolojia kupambana na utoroshaji wa madini.
Amesema Serikali imewekeza nguvu kubwa katika kuongeza uwazi kwenye mnyororo wa thamani wa madini ili kuvutia wawekezaji na kulinda maslahi ya Taifa.
Aidha, Mhandisi Kumburu ametoa wito kwa vijana wa Mkoa wa Rukwa na mikoa ya jirani kuchangamkia fursa hizo, hasa katika maeneo mapya yanayofunguliwa na Serikali.
Amesema pia Rukwa kwa sasa imeandaa mkakati wa kuweka kituo cha Mradi mkubwa wa madini ya shaba (Copper Industrial Park) katika Wilaya ya Nkasi ambapo majadiliano yanaendelea kati ya Mkoa na wawekezaji kutoka China baada ya wawekezaji kutembelea nchini na kujiridhisha na uwepo wa madini ya shaba katika Mkoa wa Rukwa na mikoa ya jirani.
“Rukwa imefunguka na sasa ni wakati wa wawekezaji kuchangamkia fursa hizi. Mazingira ya uwekezaji yameboreshwa na rasilimali zipo kwa wingi. Tunawakaribisha wote kuwekeza kwa manufaa ya Rukwa na Taifa kwa ujumla,” amesema.
Kwa ujumla, Rukwa inaendelea kupanda ngazi katika ramani ya uwekezaji Tanzania, ikiwa kama kitovu cha biashara, teknolojia na uchimbaji endelevu wa madini, huku mifumo dhabiti ya usimamizi na fursa nyingi ikiuweka Mkoa huo katika nafasi ya kipekee kwa wawekezaji wanaotafuta mazingira salama na yenye tija.

Post A Comment: