
Na Mwandishi Wetu, Handeni TC
Wenyeviti wa Serikali za Mitaa pamoja na Watendaji wa Mitaa katika Halmashauri ya Mji Handeni wamepatiwa mafunzo maalum ya uongozi na utawala bora, yanayolenga kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao, hususan usimamizi wa miradi ya maendeleo na utoaji wa huduma bora kwa wananchi.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo yaliyofanyika Desemba 1, 2025, Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Mhe. Salum Nyamwese, amewataka viongozi hao kutumia kikamilifu ujuzi walioupata ili kuboresha utendaji katika maeneo wanayosimamia.
Amesema viongozi wa mitaa wana nafasi muhimu katika kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa ubora unaotakiwa, kwa kuzingatia maslahi mapana ya wananchi na matumizi sahihi ya rasilimali.
Mhe. Nyamwese amesisitiza pia umuhimu wa kudumisha amani ya nchi, akibainisha kuwa ni urithi wenye thamani mkubwa uliopatikana kupitia juhudi za viongozi wa kizazi kilichotangulia, hivyo ni wajibu wa kizazi cha sasa kuithamini, kuilinda na kuikuza kwa ustawi wa taifa.
Awali, akifunga mafunzo hayo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Handeni, Maryam Ukwaju, amewataka Wenyeviti na Watendaji wa Mitaa kutumia mafunzo hayo kuongeza ufanisi na kuleta matokeo yenye tija katika maeneo yao ya kazi.
Aidha, amewahimiza kuzingatia weledi, uwajibikaji na uadilifu katika usimamizi wa miradi ya maendeleo, akisisitiza kuwa wananchi wana matarajio makubwa kutoka kwao katika kusukuma agenda za ustawi wa jamii.


Post A Comment: