Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, amesema kuwa Serikali inawetegemea wanasayansi na wahandisi ili kufanikisha dhamira ya Tanzania ya kujenga uchumi wa viwanda, amesisitiza kuwa kundi hilo lina mchango katika kuendeleza ubunifu, kuongeza tija na kuleta maendeleo endelevu nchini.
Prof. Mkenda amesema hayo Disemba 5, 2025 jijini Dar es Salaam katika Mahafali ya 19 ya Taasisi ya Teknolojia ya Dar es Salaam (DIT), akisema katika kutimiza azma hiyo Serikali imeendelea kuongeza fursa za mafunzo na Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi ili kusimamia ubora wa elimu sambamba na utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014, Toleo la 2023.
"Mhe Dkt. Samia Suluhu Hassan amedhamiria kuleta mageuzi ya elimu, kwa kuwawezesha watanzania hususan vijana kupata maarifa, stadi na ujuzi ili kuchangia maendeleo ya kijamii na kiuchumi" Amesema Waziri Mkenda.
Amebainisha kuwa, Serikali kupitia mkopo nafuu wa Benki ya Dunia imewekeza jumla ya Dola za Marekani milioni tisini (90) ambapo kupitia fedha hizo Taasisi ya DIT, imeanzisha Kituo cha Umahiri cha Kikanda cha Mafunzo ya TEHAMA (RAFIC) katika Kampasi ya Dar es Salaam na Kituo cha Umahiri cha Uchakataji bidhaa za ngozi (CELPAT) kampasi ya Mwanza.
Ameipongeza DIT kwa kuendelea kutoa mafunzo bora, sambamba na kutambua, kujenga, kukuza na kuendeleza bunifu. Amesema kuwa Serikali inajivunia juhudi hizo na ameisisitiza kuendelea kusimamia majukumu yake kikamilifu.
Mkuu wa Taasisi ya DIT, Profesa Preksedis Ndomba, amesema kuwa Taasisi hiyo imejikita katika dhana ya ufundishaji inayotilia mkazo mafunzo kwa vitendo pamoja na ziara za mafunzo viwandani, ambayo imewasaidia wanafunzi kuwa wabunifu na kufikia viwango vya kuanzisha makampuni.
Naye, Mwenyekiti wa Baraza la Taasisi hiyo, Dtk. Richard Masika ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutenga zaidi ya Sh. Bilioni mbili katika mwaka wa fedha 2025/26, ili kuanzisha Kituo cha Ujasiriamali, Ubunifu na Uhawilishaji wa Teknolojia kupitia Mradi wa TELM II.
Kumbuka, Mradi huo wa miaka miaka mitano (2025/2030) unatekelezwa kwa bajeti ya Euro milioni 19.79 (sawa na Sh. Bilioni 54). Fedha hizo ni mkopo nafuu kutoka Serikali ya Italia kwa Serikali ya Tanzania kupitia makubaliano rasmi.
Taasisi zingine zinazonufaika na Mradi wa TELMS II, ni Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST), Chuo cha Ufundi Arusha (ATC) na Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Karume (KIST).
Katika duru ya kwanza ya mahafali hayo, Waziri Mkenda amewatunuku vyeti jumla ya wahitimu 1,341 katika ngazi za Astashahada, Stashahada, Shahada na Shahada ya Uzamivu katika nyanja za Sayansi na Teknolojia. Kati ya hao, wanaume ni 1,003 na wanawake 338.


Post A Comment: