Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Carolyne Nombo amesema Mradi wa Airtel Smart Wasomi umekuja wakati muafaka, wakati Serikali ikitekeleza Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 Toleo la 2023 ambapo matumizi ya Tehama katika mifumo ya Elimu yamepewa kipaumbele.

Prof. Nombo amesema hayo leo Machi 22, 2024 jijini Dodoma katika halfa ya utiaji saini hati ya makubaliano ya ushirikiano wa Mradi huo kati ya Airtel, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), akisema Mradi huo utaleta faida kubwa katika sekta ya Elimu kwa kuboresha upatikanaji wa maudhui ya elimu kwa njia ya mtandao na dijitali.

Prof. Nombo ameipongeza Kampuni ya Airtel pamoja na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) kuja na Mradi huo unaoakisi malengo ya serikali katika kutoa huduma jumuishi ya Elimu kidijitali na kwamba utaongeza ari ya ujifunzaji na kuleta matokeo chanya ya ufaulu kwa Wanafunzi.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Celestine Kakele ameeleza kuwa moja ya wajibu wa msingi wa serikali ni kutoa huduma za kijamii ikiwemo elimu katika kutekeleza jukumu hilo inahakikisha usalama na utolewaji wa huduma bora na jumuishi katika Nyanja ya Mawasilino.

‘’Naipongeza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ambayo ina jukumu la kusimamia Sera na kuratibu maendeleo ya Sayansi na Teknolojia pomoja na Ofisi ya TAMISEMI ambayo inasimamia masuala ya miundombinu ya elimu kwa kushirikiana kampuni ya Airtel kutekeleza mradi huu wa kuziunganisha shule zetu na teknolojia ya mawasiliano’’ alisema Kakele. 

Akimwakilishi Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Dkt. Emmanuel Shindika amesema Mradi huo umeleta historia katika kuijenga Tanzania ya kidijitali kupitia elimu na kwamba itawasaidia Walimu kupata maudhui kwa urahisi na hivyo kuboresha ufundishaji.

‘’Malengo ya Serikali kupitia TAMISEMI ni kuhakikisha shule zetu zinakuwa na miundombinu stahiki ya utoaji elibu bora ili kufikia malengo hayo moja ya miundombinu muhimu katika karne hii ya 21 ni TEHAMA’ alisema Dkt. Shindika. 

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Airtel Tanzania Dinesh Balsingh, amesema Mradi huo utawezesha ufundishaji na upatikanaji wa maudhui kidigitali katika Shule za Serikali takriban 3,000 ndani ya miaka miatano.

Mkurugenzi huyo amebainisha kuwa Kampuni hiyo inaamini elimu ni haki ya msingi kwa kila mtoto, na hivyo inawajibika kushirikiana na Serikali kuboresha ubora wa ujifunzaji katika Shule za Sekondari Nchini ili kufikia lengo namba Nne la agenda ya maendeleo endelevu.

Nae Mwakilishi Mkazi wa UNICEF   Bi. Elke Wisch ameipongeza Serikali Tanzania kufikia hatua hiyo muhimu katika kuboresha matokeo ya kujifunza kwa kutumia huduma za kidijitali katika mfumo wa elimu.

Aidha amesema hatua ya makubaliano hayo unaifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi chache barani Afrika zenye Maktaba ya mtandaoni, na kwamba Shirika hilo litaendelea kusaidia uimarishaji wa Elimu ya kidigitali kwa kubuni mifumo rafiki na ya gharama nafuu.

Share To:

Post A Comment: