Na. Jordan Mbwambo, WF, Dodoma.
Wizara ya Fedha imewahamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika minada ya hadhara ya mali chakavu, ziada na sinzia za Serikali inayoendeshwa na Wizara ya Fedha kupitia Idara ya Usimamizi wa Mali za Serikali.
Wito huo umetolewa na Msimamizi wa Mali za Serikali Mwandamizi, Wizara ya Fedha, Bw. George Killo, wakati wa Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma 2026 yanayoendelea katika Viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma, ambapo wananchi wamekuwa wakipatiwa elimu kuhusu taratibu za usimamizi na uondoshaji wa mali za Serikali.
Alifafanua kuwa, mali zinazokuwa zimechakaa, zimepitwa na wakati au kutokuwa na matumizi tena katika taasisi za umma huondoshwa kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo husika kabla ya kuuzwa kupitia minada ya wazi inayowapa wananchi wote fursa sawa ya kushiriki.
“Tunawahimiza wananchi kufuatilia matangazo rasmi ya minada hiyo yanayotolewa kupitia vyombo mbalimbali vya habari na mifumo ya Serikali ili kupata taarifa sahihi kuhusu aina ya mali zinazouzwa, masharti ya ushiriki pamoja na ratiba za minada husika”, alisema Bw. Killo
Aliongeza kuwa, ushiriki mpana wa wananchi katika minada ya Serikali huongeza ushindani, huimarisha uwazi katika mchakato wa mauzo na huchangia katika uongezaji wa mapato katika Mfuko wa Mikopo wa Watumishi (PSAF).
Bw. Killo, alifafanua kuwa, minada hiyo huendeshwa kwa kuzingatia misingi ya usawa, haki na uwazi, ambapo kila mwananchi anayekidhi vigezo vilivyowekwa anaruhusiwa kushiriki.
Aidha, elimu inayotolewa kwa wananchi kuhusu minada ya Serikali inalenga kuongeza uelewa wa taratibu za ushiriki na kuwawezesha kutumia ipasavyo fursa zinazopatikana.
Kwa upande wa Wananchi waliotembelea Banda la Wizara katika Maonesho hayo wamepongeza juhudi za kutoa elimu kuhusu minada ya Serikali, wakieleza kuwa zimewaongezea uelewa kuhusu fursa zilizopo na kuwahamasisha kushiriki kikamilifu katika minada hiyo kwa kuzingatia taratibu na masharti yaliyowekwa.
Katibu Mtendaji wa Mamlaka ya Rufani za Zabuni za Umma (PPAA), Bw. James Sando, akiscan msimbo kupata Jarida la Hazina Yetu, linaloandaliwa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Fedha, wakati alipotembelea Banda la Wizara katika Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma 2026, yenye Kaulimbiu ya “Kuchochea Uwajibikaji Jumuishi kwa Huduma Endelevu”, yanayoendelea katika Viwanja vya Chinangali Park, jijini Dodoma.
Afisa Huduma Mwandamizi wa Hazina Saccos, Bi. Leah Nkinda, akitoa elimu kuhusuhuduma zinazotolewa na ushirika huo, kwa wananchi waliotembelea Banda la Maonesho la Wizara ya Fedha, katika Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma 2026, yenye Kaulimbiu ya “Kuchochea Uwajibikaji Jumuishi kwa Huduma Endelevu”, yanayoendelea katika Viwanja vya Chinangali Park, jijini Dodoma.








Post A Comment: