Na Mwandishi Wetu - Dodoma 


Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Bw. Lazaro Twange, amelipongeza Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA CCC), kwa mchango wake katika kupokea, kusaidia na kufuatilia utatuzi wa malalamiko ya watumiaji wa huduma za nishati na maji, hatua inayosaidia huduma zinazodhibitiwa na EWURA ikiwemo huduma ya umeme kuboreshwa kwa maslahi ya wananchi.


Bw. Twange ametoa pongezi hizo leo, Juni 19, 2026, baada ya kutembelea banda la EWURA CCC katika Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea katika Viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma.


Akizungumza katika banda hilo, Bw. Twange amesema kazi inayofanywa na EWURA CCC ya kupokea, kusaidia na kufuatilia utatuzi wa malalamiko ya huduma za umeme imekuwa chachu ya maboresho ya huduma hiyo, ikiwemo kupungua kwa baadhi ya changamoto zilizokuwa zikilalamikiwa mara kwa mara.

"Tunatambua mchango mkubwa wa EWURA CCC katika kuwawakikisha wananchi na kufuatilia utatuzi wa changamoto zao. Malalamiko mnayotupatia yanatusaidia kutambua maeneo yanayohitaji maboresho na kuchukua hatua stahiki ili kuendelea kuwahudumia wananchi kwa ufanisi zaidi," amesema Bw. Twange.


Kwa upande wake, Afisa Huduma kwa Wateja Mwandamizi wa EWURA CCC, Bw. Amani Mbogo, amesema idadi ya malalamiko yanayohusu TANESCO imeendelea kupungua ikilinganishwa na miaka iliyopita, ambapo sehemu kubwa ya malalamiko hayo yalihusiana na huduma za kuunganishiwa umeme.


EWURA CCC inaendelea kutekeleza majukumu yake ya kulinda na kutetea watumiaji wa huduma za nishati na maji kwa kutoa elimu kuhusu haki na wajibu wa mtumiaji, kupokea malalamiko ya watumiaji na kuwaelekeza utaratibu wa utatuzi wake.


Aidha, EWURA CCC imekuwa ikifuatilia malalamiko hayo ili kuhakikisha yanatatuliwa kwa wakati na mamlaka husika kwa ustawi wa watumiaji na kufanya huduma ziwe bora na endelevu.






Share To:

OKULY BLOG

Post A Comment: