Chama cha Ushirika cha Akiba na Mikopo tawi la Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya (NEW MZRH SACCOSS) leo kimetoa msaada wa mashuka 200 katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya kama sehemu yake ya huduma kwa jamii na kutambua changamoto mbalimbali ambazo hospitali inakutana nazo katika kuwahudumia wagonjwa

Akizungumza wakati wa kukabidhi Msaada huo Mwenyekiti wa NEW MZRH SACCOSS, Emmanuel Nsenye, ameutambua mchango wa Uongozi na Wataalamu wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya katika kutoa huduma bora za afya kwa wananchi na kueleza kuwa msaada huo wa mashuka 200 wenye thamani ya shilingi milioni 3 unatolewa kama sehemu ya wajibu wa NEW MZRH SACCOSS kwa jamii na kuunga mkono juhudi za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na serikali yake katika kuboresha utoaji wa huduma za afya nchini. 

“Wananchama wa New MZRH SACCOSS wametioa Msaada huu kwa kutambua umuhimu wa maendeleo ya huduma za afya hapa nchini, kurudisha kwa jamii yenye uhitaji pia kuendeleza uhusiano na ushirikiano mzuri uliopo kati ya hospitali na wadau wa maendeleo” - Nsenye

Nsenye ameonesha matumaini ya kuendelea kushirikiana na Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya na Taasisi nyingine katika kuboresha huduma za afya nchini kwa kutoa msaada utakaosaidia kupunguza changamoto katika utoaji wa huduma za afya hatua ambayo inaonesha nia njema ya NEW MZRH SACCOSS katika kusaidia kuleta maendeleo na mabadiliko chanya katika sekta ya afya nchini.

Naye Mercy D. Lutumo, Muuguzi Mkuu Msaidizi akipokea mashuka hayo kwa niaba ya Uongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya ameipongeza NEW MZRH SACCOSS kwa msaada wa mashuka na kusema kuwa msaada huo utasaidia sana kuboresha huduma za afya kwa wagonjwa na kuwashukuru Wanachama na Uongozi wa NEW MZRH SACCOSS kwa kufikiria kutoa msaada huo kwa ajili ya jamii.

Aidha, Lutumo amewahimiza wananchi na taasisi mbaimbali kuendelea kuchangia jamii zenye uhitaji ili kuweza kupunguza changamoto zilizopo katika utoaji wa huduma za kijamii, hususani huduma za afya. Amesema kwamba, kila mtu anao wajibu wa kusaidia jamii ili kufikia maendeleo na hivyo kuendelea kuwa na Taifa lenye afya bora.

“Napenda kuwashukuru Viongozi wa New mzrh saccoss kwa maono haya mazuri ya kuona hitaji la kijamii na kuona kwamba kwq hitaji hili waanze kutoka katika hospitali hii, ni jambo zuri lenye mfano wa kuigwa kwa taasisi zingine ambazo zinatoa huduma kwa jamii waone umuhimu kushiriki katika kutoa mahitaji mbalimbali kwa wahijati katika vituo vya Watoto yatima, mahospitalini ambavyo vitasaidia katika kupunguza makali ya  maisha” - Lutumo

Amesema kuwa, Uongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya unawahakikishia wananchi kuwa utaendelea kutoa huduma bora za afya kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, na hivyo kuwataka wananchi kuendelea kuitumia hospitali  kwa ajili ya kutatua changamoto zao za kiafya.

Elizabeth Satima, muuguzi katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya, amewashukuru wadau wa maendeleo, ikiwemo NEW MZRH SACCOSS, kwa msaada wa mashuka 200. Ameeleza kuwa msaada huo umekuja katika wakati muafaka kutokana na ongezeko la wagonjwa, ambalo ni matokeo ya maboresho ya miundombinu na upanuzi wa huduma za afya.

Elizabeth Satima ametoa wito kwa wadau wengine kuiga mfano wa NEW MZRH SACCOSS kwa kutoa misaada kwa hospitali na jamii zenye uhitaji. Amewahakikishia wadau hao kwamba msaada huo utatumika ipasavyo na utaleta mabadiliko chanya katika utoaji wa huduma za afya kwa wananchi.

Share To:

Post A Comment: