RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan ametoa zaidi ya shilingi bilioni 20 kutekeleza miradi ya maji katika Halmashauri ya wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma.


Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Maji Mhandisi Maryprisca Mahundi wakati wa uwekaji jiwe la msingi mradi wa maji katika Kijiji cha Hongi Kata ya Liuli wilayani Nyasa ambao umegharimu shilingi bilioni 4.7.

Ameitaja baadhi ya miradi inayoendelea kutekelezwa katika wilaya hiyo kuwa ni mradi wa maji Mwerampya kata ya Lituhi unaogharimu shilingi bilioni 6.5,mradi wa maji Kilosa Mbambabay unaogharimu zaidi ya shilingi bilioni 4 na mradi wa maji Ngumbo unaogharimu shilingi bilioni 2.5.

“Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ni mwanamama aliyedhamiria kumtua mama ndoo kichwani kwa vitendo,Wizara ya Maji imejipanga usiku na mchana kuhakikisha maji safi na salama yanafika kwa wananchi wote wa Tanzania’’,alisisitiza Waziri Mahundi.

Ametoa rai kwa wananchi wa wilaya ya Nyasa wanaofanya shughuli za kibinadamu kwenye vyanzo vya maji ikiwemo mito kuacha mara moja tabia hiyo kwa kuwa inasababisha madhara makubwa kimazingira ikiwemo mafuriko hivyo kuathiri makazi ya watu.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas amesema asilimia 70 ya watu wanaoishi vijijini mkoani Ruvuma ambao ni 1,294,156 kulingana na sensa ya watu yam waka 2022 wanapata huduma yam aji safi na salama ambapo lengo la Mkoa kufikia asilimia 85 kupata maji safi na salama kwa wakazi wa vijijini ifikapo mwaka 2025.

Amesema vijiji 373 kati ya vijiji 533 vinavyohudumiwa na Wakala wa Maji vijijini RUWASA mkoani Ruvuma vinapata maji safi na salama na kwamba hadi kufikia Juni 30,2023 Mkoa wa Ruvuma ulikuwa unatekeleza jumla ya miradi 33 yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni zaidi ya bilioni 55.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Nyasa Mhandisi Stella Manyanya ameishukuru serikali kwa kuendelea kupeleka fedha nyingi za miradi ya maendeleo katika jimbo la Nyasa ikiwemo miradi ya maji iliyojengwa kwa viwango vya juu.

Hata hivyo amesema mradi huo wa maji wa Liuli unakwenda kumaliza kero yam aji ya muda mrefu ambayo walikuwa wanaipata wananchi wa Kata hiyo na vijiji jirani.
Share To:

Post A Comment: