Mwanasheria Eliakim Paulo kutoka Shirika la Civil Social Protection Foundation (CSP) akizungumza na Wanawake wajasiriamali, Wasaidizi wa sheria na Waandishi wa Habari katika mji mdogo wa Mirerani.
Vikundi vya wanawake wajasiriamali kutoka Mamlaka ya mji mdogo wa Mirerani wakisikiliza mada mbalimbali zinazowasilishwa kwenye Mafunzo ya kuwajengea uwezo yanayosimamiwa na shirika lisilo la serikali la Civil Social Protection Foundation (CSP).



Na John Walter-Manyara

Wanawake wajasiriamali wa Madini katika Mamlaka ya mji mdogo wa Mirerani wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara, wamelipongeza shirika lisilo la serikali la Civil Social Protection Foundation (CSP) kwa kuwasaidia kutambua haki zao.

Mwenyekiti wa Sunshine Group, Fatuma Kifunta anakiri awali walikuwa wakifanyiwa udhalilishaji kwa kupekuliwa kwa kuvuliwa nguo wakati wa kuingia na kutoka ndani ya ukuta wa Mgodi wa Tanzanite,  lakini baada ya Shirika hilo kuwapa elimu na kuwajengea uwezo na kujua namna ya kutafuta haki zao  jambo hilo kwa sasa halipo.

Kifunta ameipongeza Serikali kwa kuzuia uuzwaji holela wa Madini ya  Tanzanite huku wakiomba iendelee kusimamia msimamo wake wa kuuza madini hayo ndani ya Mirerani Pekee.

Amesema  "Nyumba nyingi zilizokuwa zinapangishwa hapa Mirerani zimebaki bila watu kwa kuwa wanunuzi waliokuwa wanatoka maeneo mbalimbali kufika kununua madini hayo wamehama kutokana na utaratibu uliopo"

Amesema Mji huo haujengeki kwa sababu wachimbaji wengi na wafanyabiashara wamefanya ni kama njia ya kupita hivyo serikali ihakikishe makao makuu ya Tanzanite ni Mirerani pekee na sio kwingine ili kuwavuta wafanyabiashara hao.

Afisa maendelo ya Jamii wa mji mdogo wa Mirerani Isaack Mgaya akifungua Mafunzo hayo amelipongeza shirika la CSP akieleza kuwa limetoa mchango mkubwa sana kwa serikali kumaliza changamoto mbalimbali zilizokuwa zinawakabili wanawake wanaofanya shughuli zao katika Mgodi wa Tanzanite vikiwemo vitendo vya ukatili wa kijinsia.

Amesema uchumi wa Mirerani unabebwa na Madini ya Tanzanite ambayo yanachimbwa na Wanaume lakini masuala ya kijamii haswa familia, yanabebwa na Wanawake wajasiriamali wadogo wadogo.

"Kwa hiyo kuwajengea uwezo Wakina mama katika masuala mbalimbali yanayowahusu ni kuiokoa Jamii ya Mirerani, kuwaokoa watoto ambao ndio taifa la kesho"

Mradi wa kuwajengea uwezo Wanawake katika masuala ya Uchumi unaojulikana kwa jina la "Tanzanite kwa Uchumi Imara wa Wanawake" kwa lengo la kuwaufaisha Wanawake wanaofanya kazi ndani ya ukuta unaozunguka mgodi wa Tanzanite umewaunganisha pia waandishi wa Habari na wasaidizi wa sheria ambao watasaidia kupaza sauti pindi panapotokea changamoto mbalimbali ikiwemo ukatili wa Kijinsia.

Mwanasheria Eliakim Paulo kutoka Shirika la Civil Social Protection Foundation (CSP) amesema Lengo la Mradi huo ni  kuweza kuwafundisha wanawake wajasiariamali  na kuwajengea uwezo wa kuweza kuripoti changamoto zinazowakabili wakiwa kwenye shughuli zao, waandishi wa habari  pamoja na wasaidizi wa sheria. 

Katibu wa chama cha wachimbaji Madini (MAREMA) Tawi la Mirerani mkoani Manyara Rachel Njau, amesema Mirerani itakuwa kama Arusha kwa maendeleo endapo viongozi wataamua kusimama imara na kuacha ubinafsi.

Mwezeshaji katika mafunzo hayo ya siku nne kaimu mkurugenzi wa shirika la Biashara na Haki za Bindamu Tanzania (BHRT) Rose Ugulumu amesema tatizo ni jamii kukosa elimu ya moja kwa moja juu ya masuala ya uwekezaji, haki zao pamoja na  sheria wanazopaswa kuzifuata na kwamba ifike mahali jamii izingatie na kujikumbusha sera za Ujamaa na kujitegemea iliyoasisiwa na waasisi wa nchi, jamii moja ikifanikiwa na wengine wananufaika.


Share To:

Post A Comment: