Chuo Cha Uhasibu Arusha (IAA) kimezindua rasmi Dawati la Jinsia likiwa na dhumuni kuelimisha Wanafunzi, Wafanyakazi pamoja na watoa huduma katika Chuo kuhusu umuhimu wa kuzingatia masuala ya kijinsia katika shughuli zao za kila siku.

Akizindua dawati hilo Mkuu wa Chuo-IAA Prof. Eliamani Sedoyeka amesema dawati litawasaidia wadau hao kupata elimu juu ya unyanyasaji na ukatili wa kijinsia, hatua za kuzuia vitendo hivyo na namna ya kushughulikia endapo vitendo hivyo vitajitokeza.

“ Mtakapoona vitendo vyovyote vinavyoashiria unyanyasaji na ukatili wa kijinsia toeni taarifa kwa namna mtakavyoona inafaa ili mpatiwe msaada wa namna mbalimbali ikiwemo msaada wa kisaikolojia, msikae kimya,” amesema Prof. Sedoyeka.

Prof. Sedoyeka ameongeza kuwa uongozi wa Chuo utaendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali ikiwemo, TAKUKURU, Dawati la jinsia la Polisi, Ofisi ya Mwendesha mashtaka wa serikali, pamoja na vyombo vingine katika suala la kuzuia na kupambana na ukatili wa kijinsia ili kuhakikisha IAA inakuwa sehemu salama.

Akiwasilisha mada Mratibu wa jinsia na maendeleo ya mtoto Jiji la Arusha Bi. Habiba Madebe amezitaja baadhi ya sababu zinazopelekea ukatili wa kijinsia katika jamii kuwa ni pamoja na mila, desturi, mmomonyoko wa maadili na mfumo dume, huku akisisitiza kuwa wako mstari wa mbele katika kupambana na ukatili huo.

Naye mwakilishi kutoka Dawati la jinsia la Polisi Arusha Sajenti Restituta ameeleza kuwa Jeshi la Polisi limekuwa  mstari wa mbele katika kupambana na ukatili wa kijinsia hasa mashuleni, vyuoni na katika jamii kwa ujumla na wamekuwa wakiwachukulia hatua wale wote wanaojihusisha na ukatili huo.

Anyesi Mkolelwa ni mwanafunzi wa IAA aliyeshiriki katika uzinduzi huo, ameushukuru uongozi wa Chuo kwa kuanzisha dawati hilo, kwani utawasaidia wao kama wanafunzi kupata elimu na kuwa wa kwanza kuzuia na kupambana na ukatili wa kijinsia hasa wakiwa Chuoni.

Uzinduzi huo umefanyika leo IAA ukihudhuriwa na wanafunzi, wafanyakazi wa Chuo, watoa huduma, wawakilishi kutoa taasisi mbalimbali,pamoja wa wadau wengine.Share To:

Post A Comment: