Wafanyabiashara wadogowadogo nchini, maarufu kama Machinga,wamekuwa wakimshukuru na kumpongeza Rais wa Awamu ya sita, Samia Suluhu Hassan, kwa kuwatengea maeneo maalum ya kufanyia biashara zao katika kila Halmashauri nchini. Hata hivyo, hali ni tofauti katika Halmashauri ya Karatu, Mkoani Arusha, ambapo wamachinga wa wilaya hiyo hawana soko la kufanyia biashara.

Soko hilo, ambalo mpaka sasa limeshagharimu zaidi ya Milioni 27, lipo chini ya kiwango. Awali, Shilingi Milioni 15 zilitumika kujenga choo chenye matundu manne.Aidha, Milioni 12 zilitumika kuevua baa katika soko hilo na kuweka nguzo, lakini meza za kuuzia bidhaa hazijajengwa.

Teddy Mathew, mkazi wa Kata ya Karatu, amesikitishwa na kitendo cha Halmashauri kushindwa kukamilisha soko hilo, hivyo kuwaacha wamachinga bila maeneo ya kufanyia biashara na wananchi kukosa eneo maalum la kupata bidhaa za machinga. Anashangazwa na gharama ya ujenzi wa choo,ambayo inasemekana kuwa Milioni 15.

Anaongeza, "Nafahamu Rais wetu ni msikivu sana na anapenda wamachinga.Namuomba awaangalie wafanyabiashara wa Karatu. Wanateseka sana na wamekuwa kama wamesahaulika kabisa. Hakuna chochote kinachoendelea hapa, eneo limeanza kuwa kama kichaka sasa."

Hashim Bakari, mfanyabiashara mdogo (machinga) katika Wilaya ya Karatu, anasisitiza kwamba mradi wa soko hilo umekuwa ukijengwa chini ya kiwango. Anatoa mfano wa masoko mengine katika wilaya nyingine na mitandao ambayo yamejengwa kwa mtindo wa kisasa.

"Serikali yetu inapaswa kuwachukulia hatua mara moja watumishi wote wa halmashauri waliohusika kuhujumu ujenzi wa soko letu hili, pamoja na ujenzi wa choo kilichogharimu Milioni 15. Thamani ya fedha haiendani na kazi iliyofanyika," anasema Hashim.

Mbunge wa Jimbo la Karatu, Daniel Awack, anasema ameomba mchoro wa soko hilo ili aweze kutoa fedha kiasi cha shilingi milioni nane. Hata hivyo, amekuwa akisubiri mchoro huo kwa zaidi ya wiki tatu bila kupewa majibu.

Kwa kuwa Bunge la Bajeti linaendelea, na siku chache zimebaki kabla ya mwaka wa fedha wa Serikali kumalizika, ana wasiwasi kuwa fedha zilizotengwa kwenye mfuko wa jimbo zitarudishwa kutokana na kukosekana kwa mchoro uliopitishwa na Halmashauri ya Mji mdogo wa Karatu ili kuanza ujenzi wa soko hilo.

Awack anasema, "Hakuna soko la machinga. Haiwezekani shilingi milioni 12 zitumike kujenga soko hili ambalo thamani ya fedha haiendani na kazi iliyofanyika, hasa kwenye choo."

Mwenyekiti wa Mamlaka ya Mji mdogo wa Karatu, Yuda Morata, anasema walikubaliana katika kikao kwamba soko hilo liwe na nguzo za chuma, lakini badala yake halmashauri imeweka nguzo za mbao. Pia, choo kilichojengwa kimetumia vifaa vilivyobaki kutoka kwenye nyumba za watumishi ya 3-in-1 ambazo ni za wakuu wa idara na bado hazijakamilika.

Morata anaongeza, "Ramani iliyojengwa pale kwenye lile soko siyo ramani tuliyokubaliana. Nina mashaka pia kama kuna ramani ya soko, kwa sababu tulichokubaliana kwenye kikao sio kilichojengwa.Fedha zilizotumika kwenye ujenzi wa soko hili ni nyingi ikilinganishwa na kazi iliyofanyika."

Katibu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Karatu, Ramadhan Juma, anasema mradi huo umefanywa kwa usiri mkubwa. Uongozi wa machinga na viongozi wa kata hawakushirikishwa kuhusu mradi huo, na wanapohoji, hawapati majibu kutoka kwa Mhandisi.

"Machinga wanapata tabu. Wanazunguka mjini wakati serikali imetenga fedha za kuwajengea soko. Sisi viongozi tunaulizwa na machinga kila siku ni lini soko litakamilika, lakini hakuna majibu. Hatujashirikishwa kwenye mradi huu, hali inayosababisha kukosa majibu ya kuwapa wananchi wengine wanaohitaji huduma za machinga." anasema Juma.

Anaongeza, "Niiombe serikali sikivu kuhakikisha kuwa wanapofanya mradi wowote, wanashirikisha hata viongozi wa kata ili tufahamu kinachofanyika katika eneo husika. Hivyo, tunaweza kuelezea kwa wananchi vyema kinachofanyika wakati wa mikutano yetu ya kata."

Ni muhimu kukumbuka kwamba tarehe 13 Septemba 2021, Rais Samia Suluhu Hassan aliwataka wakuu wa mikoa nchini kuwapanga wamachinga katika maeneo stahiki bila kusababisha vurugu. Rais Samia alielezea kuwa, ingawa serikali inatoa fursa ya kufanya biashara kwa njia ya ajira kwa machinga, wamekuwa wakifanya kazi katika maeneo tofauti na kuziba maduka ya watu.

Aliagiza wakuu wa mikoa kuchukua hatua za kuwapanga vizuri na kuwaweka machinga bila kuingilia shughuli za wenye maduka, ili kuendeleza amani na maisha bora.










Share To:

Post A Comment: