‎Na Edward Winchislaus.

MBUNGE  wa Jimbo la Mtumba na Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, amemkabidhi nyumba iliyofanyiwa ukarabati Bi. Verian Mlewamwenye umri wa miaka 75, mkazi wa Kata ya Mtumba jijini Dodoma, ambaye alikuwa katika hatua ya kuiuza nyumba yake kwa Shilingi 500,000 ili kupata fedha za matibabu baada ya kuugua uvimbe katika ubavu.

Hatua hiyo imefuatia taarifa za hali ya bibi huyo kuripotiwa kwenye vyombo vya habari, ambapo kwa kushirikiana na Kitengo cha Ustawi wa Jamii, Bi. Verian alipelekwa Hospitali ya Rufaa ya Dodoma na kufanyiwa upasuaji uliomwezesha kurejea katika hali nzuri ya afya.

‎Akizungumza na wananchi wa Mtaa wa Vikonje B, Kata ya Mtumba, wakati wa kukabidhi nyumba hiyo leo, Desemba 26, 2025, Mhe. Mavunde amesema kuwa aliguswa na simulizi ya maisha ya bibi huyo baada ya kuona taarifa zake kwenye vyombo vya habari.

‎“Nimeona nitumie fursa hii kuikabidhi nyumba iliyofanyiwa ukarabati. Nyumba hii ni ya Bi. Verian aliyeijenga mwenyewe. Baada ya kuona taarifa kuwa anaumwa na kukosa fedha za matibabu hadi kufikia hatua ya kutaka kuuza nyumba yake, tulishirikiana na ofisi ya ustawi wa jamii kumpeleka hospitalini, akafanyiwa upasuaji na kupona,” amesema Mhe.Mavunde

Aidha Mavunde ame‎ongeza kuwa baada ya Bi. Verian kupona, waliamua kuikarabati nyumba hiyo ili aishi katika mazingira salama na yenye staha.

“Tuliamua kuikarabati nyumba hii ili bibi aishi maisha bora na ya furaha. Rai yangu ni kuwaona wanajamii wakirejesha tabasamu kwa waliopoteza matumaini, kwani hii ni sadaka kubwa mbele ya Mwenyezi Mungu,” amesisitiza Mhe.Mavunde Katika ukarabati huo, madirisha yaliyokuwa yamezibwa kwa matofali yaliondolewa na kuwekwa madirisha ya kisasa ili kuruhusu mwanga na hewa kuingia ndani. Mbali na ukarabati wa nyumba, Mhe. Mavunde amemkabidhi Bi. Verian msaada wa mahitaji mbalimbali ikiwemo kilo 80 za sukari, mchele, mafuta ya kupikia, maji, pamoja na vitenge na kanga. Aidha, Mhe. Mavunde amebainisha kuwa watamuwezesha Bi. Verian kupata mtaji kwa kumjengea mabanda ya kuku ili afuge kuku wa kienyeji na kujiendeleza kiuchumi.

Kwa upande wake,Afisa Ustawi wa Jamii wa Kata ya Mtumba, Bi. Mela Katamba,amesema kuwa walipokea taarifa za dhamira ya Bi. Verian kuuza nyumba yake na kuchukua hatua za haraka kufanya uchunguzi wa karibu.

“Tulibaini changamoto yake kubwa ilikuwa kupata matibabu. Kwa kuwa alikuwa na zaidi ya miaka 60, alikidhi vigezo vya kupata msamaha wa matibabu, hivyo tulimpeleka hospitalini na akapatiwa huduma stahiki,” amesema

Ameongeza kuwa baada ya matibabu, waliendelea kushirikiana na Mhe. Mavunde ambaye alimhudumia Bi. Verian kwa kumpatia kitanda na godoro kabla ya kutekeleza ahadi ya kukarabati nyumba yake.

Naye Bi. Verian Mlewa amemshukuru Mhe. Mavunde kwa msaada huo akisema umebadilisha maisha yake na kumpa matumaini mapya baada ya kipindi kigumu alichopitia. Awali  Mwanawe, Bi. Abigail Daud (40), amema familia ilikabiliwa na changamoto kubwa ya kugharamia matibabu ya mama yao kutokana na hali duni ya kipato.

Share To:

Alex Sonna

Post A Comment: