NA DENIS CHAMBI, TANGA.

 Shirika  la Next Einstein Forum (NEF) kwa kushirikiana na kituo cha sayansi cha Stem Park pamoja na halmashauri ya jiji la  Tanga limetoa tuzo kwa walimu 10 wa kike wa shule za msingi na sekondari waliofanya  vizuri katika ufundishaji wa masomo ya sayansi na hisabati  hii ikiwa  na lengo la kuongeza  motisha ya ufundishaji ili kuandaa wanafunzi mahiri watakaoingia kwenye soko la kiushindani wa ajira pamaoja na wataalamu mbalimbali wa baadaye.

Tuzo hizo zilikabidhiwa leo june23,2023 na mkurugenzi wa halmashauri ya jiji la Tanga Dkt.Sipora Liana kwa walimu watano wa shule za msingi na watano wa shule za sekondari.

Dkt. Liana aliwapongeza walimu hao kwa kuendelea kutekeleza majukumu yao ya kitaaluma yanayoendana sambamba na malezi bora kwa watoto huku akiwataka kuwa mabalozi kwa walimu wengine  kwaajili ya kuandaa taifa lenye watu wema ,waadilifu na wenye kusimamia maadili mema.

Aidha mkurugenzi huyo amewapongeza NEF pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo hasa katika sekta ya elimu kwa jitihada wanazoendelea kuzifanya kwaajili ya kuhakikisha kiwango cha taaluma kinakuwa kwa kuweka miundo mbinu mbalimbali ikiwemo ujenzi wa madarasa , madawati pamoja na kuweka mazingira rafiki ya kujifunzia na kufundishia.

“Hongereni sana walimu wote hasa walimu wa sayansi kwa kazi kubwa mnayofanya katika kutimiza wajibu wenu wa kuwafundisha watoto wetu na kuwaandaa katika misingi bora mnafanya kazi kubwa sana mnahitaji pongezi endeleeni kuwapa motisha watoto wetu, tunawapongeza sana wadau wote ambao tunasaidiana nao hasa kupitia sekta ya elimu kwa kujenga na kuboresha  miundominu mbalimbali  ya elimu “ alisema Dkt. Liana.

Akizungumza balozi wa shirika la Next Einstein Forum (NEF) Dkt. Isaya Ipyana alisema kuwa tuzo hizo walizozitoa kwa walimu wa kike wanaofundisha masomo ya sayanasi katika shule za msingi na sekondari ni katika kuwaongezea ari ya ufundishaji ili kuongeza ufanisi pamoja na kuwaandaa wanafunzi wenye uwezo mkubwa kitaaluma.

Dkt Ipyana aliwataka wazazi, walezi na jamii kwa ujumla kuwalea watoto katika misingi bora ya kimaadili sambamba na kuwapa nafasi ya kupenda kujifunza masomo ya sayansi ambayo yana nafasi kubwa ya ajira katika ulimwengu wa sasa.

“Tuzo hizi zilizoandaliwa na NEF kwa kushirikiana na kituo cha sayansi cha Stem Park pamoja na halamashauri ya jiji la Tanga ni kwaajili ya kuwapatia motisha walimu wa kike wanaofundisha masomo ya sayansi na hisabati katika shule za msingi na sekondari , niwaase sana wazazi na walezi kuwalea watoto wao katika mazingira bora na kupenda kujifunza masomo ya sayansi kwani ndio yenye tija katika ulimwengu wa sasa  unaoenda kidigital.” alisema Dkt. Ipyana.

Awali akizungumza afisa maendeleo ya jamii Simon Mdende amesema pamoja na jitihada mbalimbali wanazozifanya  walimu kupitia sekta ya elimu ni vyema wakatambua kuwa wanalo jukumu kubwa la malezi kwa watoto pindi wanapokuwa mashuleni katika kuhakikisha wanasimamia maadili mema pamoja na kuwaepusha na vitendo vya ukatikatili

“Pamoja na kuwa walimu mnafanya vizuri  kitaaluma katika masomo hasa ya sayansi lakini nisistize kwamba ulimwengu wa sasa umebadilika sana naomba tuhakikishe tunawalea watoto wetu katika maadili mazuri , tuwakinge na maadili mabaya yanayopelekea mmomonyoko wa maadili hasa maswala ya ukatili wa kijinsia” alisema Mdende.

Mmoja walimu waliopata tuzo hizo akipeana mkono na afisa maendeleo ya halmashauri ya jiji la Tanga Simon Mdende.
Mkurugenzi wa jiji la Tanga Dkt Sipora Liana ( wa pili kulia waliokaa )akiwa na walimu waliopata tuzo hizo zilizoandaliwa na NEF kwa kushirikiana na kituo cha sayansi Stem Park pamoja na halmashauri ya jij la Tanga.
Balozi wa wa shirika la Next Einstein Forum (NEF) Dkt. Isaya Ipyana akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya hafla hiyo ya kukabidhi tuzo kwa walimu wa kike wa shule za msingi na sekondari wanaofundisha masomo ya sayansi na hisabati.
Baadhi ya watumishi wa kituo cha Stem Park wakiwa kwenye picha ya pamoja na mkurugenzi wa jiji la Tanga Dkt Sipora Liana mara baada ya shughuli hiyo.
 

Share To:

Post A Comment: