Na Respice Swetu.

Zikiwa zimetimia siku zilizotolewa na Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa watumishi wapya wa kada ya ualimu na afya kuripoti katika halmashauri walizopangiwa, jumla ya walimu 139 wameripoti katika halmashauri ya Wilaya ya Kasulu.

Akitoa taarifa ya kuripoti kwa walimu hao, Katibu wa Tume ya Utumishi wa Walimu Wilaya ya Kasulu Samwel Rubamba amesema, idadi hiyo inajumuisha walimu wa shule za msingi na sekondari.

Amesema, halmashauri ya Wilaya ya Kasulu iliyopangiwa walimu 143 kati yao 115 wakiwa ni wa shule za msingi na 28 wa shule za sekondari, hadi kufikia Juni 22 muda ambao wanatakiwa wawe wamekwisharipoti, walimu 139 ndio walioripoti.

Amefafanua kuwa kati ya walimu hao, walimu 113 ni walimu wa shule za msingi na 26 wakiwa ni walimu wa shule za sekondari.

"Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu ilipangiwa walimu 143 wa ajira mpya ambapo hadi jana waliokuwa hawajaripoti ni walimu wanne tu ambapo kati yao wawili ni wa shule za msingi na wengine wawili wakiwa ni wa sekondari", amesema.

Rubamba amewataja walimu ambao hawajaripoti na shule walizopangiwa kuwa ni Adeliph Bwemero wa Kamembe na Sukaina Gulamali wa Rusesa huku Adam Msigwa na Ramadhan Samatta wakiwa ni wa shule ya sekondari ya Kamuganza. 

Kuhusu hatima ya walimu ambao hawajaripoti amesema, pamoja na kuwa walipewa muda maalumu wa kuripoti  kwenye halmashauri zao uliotamatika jana, ofisi ya elimu imefanya kazi kubwa ya kuwatafuta bila mafanikio.

"Tumeshirikiana na maafisa elimu kuwatafuta walimu hao kwa kuwapigia simu na kwa njia mbalimbali bila mafanikio, nitumie nafasi hii kuwaasa walimu hao wajitokeze kuja kunusuru ajira zao", amesema.

Akitangaza ajira hizo mapema mwezi huu, Waziri wa Ofisi ya Rais Tamisemi Anjella Kairuki, aliwataka waajiriwa hao wawe wameripoti kwenye halmashauri walizopangiwa katika muda uliowekwa ambao umekamilika Juni 22 mwaka huu.
Share To:

Misalaba

Post A Comment: