Mwenyekiti wa Bodi ya Kahawa Tanzania Prof.Aurelia Kamuzora akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya majadiliano katika mkutano mkuu wa 13 wa wadau wa Kahawa hapa Nchini Leo Juni 21,2023 jijini Dodoma.

Na Okuly Julius-Dodoma

BODI ya Kahawa Tanzania ,imesema tangu uhuru kahawa haijawahi kuzalishwa kwa wingi kama mwaka huu ambapo uzalishaji umefikia tani 82,000 na mikakati iliyopo ni kufikia tani 300,000 Kwa miaka ijayo.


Hayo yameelezwa na Mwenyekiti wa Bodi hiyo Prof.Aurelia Kamuzora wakati akizungumza kwenye mkutano mkuu wa 13 wa wadau wa Kahawa hapa Nchini Leo Juni 21,2023 jijini Dodoma.


“Tangu uhuru kahawa haijawahi kuzalishwa kwa wingi kama mwaka huu tumefikia uzalishaji wa tani 82,000 yajayo yanafurahisha na mikakati iliyopo ni kufikia tani 300,000 tunaona lengo linakwenda kutimia,”alisema.

Pia Prof.Aurelia amewaomba wakulima wa mikoa inayolima zao hilo kukubali makato ya Sh.213 kwa kilo kwa ajili ya kuchangia Mfuko wa uendelezaji Kahawa na kuchochea uzalishaji wake.


Amesema kupitia fedha hizo Bodi inarudisha maendeleo kwa wakulima ikiwamo kupeleka miche na kusaidia huduma za ugani.


“Niwahakikishie wakulima mchanganuo wa fedha hii ya makato tumeweka wazi na hakuna fedha itakayopotea, tuna mikakati mingi ya kuhakikisha kahawa ya Tanzania inaendelea kusifika kwa ubora wake,”alisema.


Amesema Mkoa wa kagera wamekubali makato na kuwaomba Wakuu wa Mikoa, Wilaya na Wabunge kusaidia kuhamasisha wakulima wa maeneo yao kukubali.


Amesema mafanikio yaliyopatikana kutokana na mikakati ya bodi ya kukwamua zao hilo ni pamoja na kuiingizia nchi fedha za kigeni ambapo kwa msimu uliopita zao hilo liliingiza zaidi ya Dola za Marekani milioni 200.


Amewaomba wakulima kuendelea kulima zao hilo kwa kuwa ni mali na Bodi itahakikisha inatumia makato hayo kutafuta miche ili wapande zaidi.


Naye, Mratibu wa Mradi wa kuboresha na kuendeleza zao la kahawa kwa wakulima wadogo wa nyanda za juu kusini kutoka Shirika la Viagroforestry, Rashid Malya, alisema shirika hilo linatekeleza mradi wa CODE-P wa miaka minne ulianza mwaka 2020 na utahitimishwa Mei 2024 ambao unalenga kuchochea uwekezaji wa sekta binafsi katika mnyororo wa thamani wa zao hilo, kuongeza ajira na kuboresha usalama wa chakula na lishe kwa wakulima wadogo.


Alieleza kuwa lengo la mradi ni kufikia wakulima 24,000 katika wilaya sita za mikoa mitatu ya Mbeya, Songwe na Ruvuma ambapo hadi sasa walifikiwa ni 21,000 huku wanaume wakitajwa kujishughulisha zaidi katika uzalishaji kuliko wanawake.


Akizungumzia kuhusu tija na uzalishaji endelevu wa kahawa aina ya robusta mkoani Kagera, Mwakilishi Shirika la Café Africa, Samora Mnyaonga, alitaja vikwazo wanavyokubana navyo wakulima kuwa ni kukosa fursa ya kupata mikopo kwa ajili ya kugharamia uendeshaji wa mashamba yao ya kahawa huku akitolea mfano mikopo ya pembejeo za kilimo.
Share To:

OKULY BLOG

Post A Comment: