Na Jacquiline Mrisho - MAELEZO

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Innocent Bashungwa, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuzipa kipaumbele shughuli za ulinzi kwa kutoa fedha kugharamia shughuli hizo.

Shukrani hizo zimetolewa leo bungeni jijini Dodoma na Waziri Bashungwa wakati akiwasilisha hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha ya wizara hiyo kwa mwaka 2023/24 ambapo amempongeza Rais Samia kwa juhudi zake za dhati katika kuhakikisha Taifa linaendelea kuwa na umoja, amani, utulivu, ustawi na kasi ya maendeleo ya kiuchumi.

“Tunamshukuru Rais Samia kwa kuendelea kuzipa kipaumbele shughuli za ulinzi kwa kutoa fedha kugharamia operesheni za kupambana na ugaidi, ujenzi wa Makao Makuu ya Ulinzi wa Taifa – Kikombo Jijini Dodoma, kusafirisha wastaafu, madeni ya wazabuni, mafunzo na vifaa vya mifumo ya malipo na ununuzi wa magari ya makamanda na Wambata Jeshi”, alisema Bashungwa.

Vilevile kwa niaba ya Serikali, Bashungwa amezishukuru nchi rafiki kwa ushirikiano wao katika shughuli za Ulinzi, nchi hizo ni pamoja na Algeria, Bangladesh, Ethiopia, Finland, Ghana, Hispania, Indonesia, Israeli, Jamhuri ya Czech, Jordan, Misri, Morocco, Nigeria, Oman, Pakistan, Serbia, Sri Lanka, Sweden, Uholanzi, Uingereza, Umoja wa Falme za Kiarabu, Urusi, na Uswisi.

Kwa upande mwingine, Bashungwa ameeleza kuwa kwa mwaka wa fedha 2022/2023, hali ya ulinzi na usalama wa mipaka ya nchi yenye urefu wa kilomita 5,461.20, ambayo inahusisha eneo la nchi kavu linalopakana na nchi nane na eneo la maji, hususan Bahari ya Hindi linalopakana na nchi za Comoro na Shelisheli imeendelea kuwa shwari na hapakuwa na matukio ya uhasama baina ya Tanzania na nchi zinazopakana nazo.

Wizara kwa mwaka wa fedha 2022/2023, imefanikiwa kutekeleza shughuli mbalimbali kwa kutumia fedha zilizotolewa kwa ajili ya matumizi ya kawaida zikiwemo za mafunzo na mazoezi ya kijeshi, mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa, mafunzo ya Jeshi la Akiba, matunzo ya zana na vifaa vya kijeshi, huduma za afya na tiba, ushirikiano na mamlaka za kiraia, ushirikiano wa kiulinzi na nchi nyingine, ushiriki wa Jeshi katika michezo, mapambano dhidi ya magonjwa ambukizi na yasiyoambukiza, utawala bora na utunzaji wa mazingira.


Share To:

Post A Comment: