Na,Jusline Marco:Arusha

Zaidi ya asilimia 70 ya wangojwa wa saratani wanaofika kwenye taasisi ya saratani ya Ocean road kwa ajili ya matibabu ni wanawake ukilinganisha na idadi ya wanaume huku zaidi ya 75 ya wagonjwa hao wanafika kupata huduma wakiwa katika hatua kubwa za ugonjwa.

Meneja wa Kitengo cha Uchunguzi wa Saratani na Elimu kwa Umma kutoka katika Taasisi ya Saratani Ocean road ya Jijini Dar es salaam Dkt.Maguha Stephano ,ameyasema hayo katika Kambi ya uchunguzi na matibabu ya saratani inayoendeshwa na taasisi ya saratani ya ocean road kwa kushirikiana na hospital ya rufaa ya Mkoa wa Arusha mountmeru.

Akizungumza na waandishi wa habari kwenye kambi hiyo ambayo imefanyika katika hospitali ya rufaa ya Mountmeru, Dkt.Maguha amesama kuwa takwimu za mwaka 2021 saratani ambayo imeongoza kwa wagonjwa wengi kwa upande wa akina mama ni saratani ya mlango wa kizazi kwa asilimia 47.

"Ikiwa na maana kwamba kati ya wagonjwa 100 wenye saratani, wagonjwa 47 wana saratani ya mlango wa kizazi,saratani nyingine ni saratani ya matiti kwa asilimia 18 na mwisho ni saratani ya koo la chakula,kwahiyo hizi ndizo saratani ambazo zinaongoza kuwa na wagonjwa wengi."alisema Dkt.Maguha Meneja wa Kitengo cha Uchunguzi wa Saratani na Elimu kwa Umma kutoka katika Taasisi ya Saratani Ocean road

Aidha aliongeza kuwa kwa upande wa wanaume saratani inayoongoza kuwa na wagonjwa wengi ni saratani ya koo la chakula kwa asilimia 18,ikifuatiwa na saratani ya tezi dume ikiwa na asilimia 11 huku ya mwisho ikiwa ni saratani ambazo zipo katika maeneo ya kichwani n shingoni.

"Changamoto tunayoipata kwenye taasisi yetu ni wagonjwa wanaofika kupata matibabu ya saratani wanakuwa katika hatua kubwa ya ugonjwa nikimaanisha hatua ya tatu naya nne ambayo ugonjwa unakuwa ni ngumu kuutibu hivyo inatupasa kupunguza madhila ambayo yanaambatana na ugonjwa wa saratani lakini siyo kutibu kabisa."slisema Dkt.Maguha

Kufuatia hali hiyo Taasisi ya Saratani ya Ocen road kwa kushirikiana na Wizara ya Afya imeamua kuandaa mpango wa kufika katika hospitali za rufaa za mikoa nchini ili kutoa elimu na huduma za uchunguzi za awali za saratani ikiambatana na kufanya ugunduzi wa mapema wa saratani katika hatua za awali ambapo kampeni hizo zinakuwa zimeambatana na wataalam wa uchunguzi,madaktari bingwa wa saratani pamoja na madaktari bingwa wa vipimo vya kugundua saratani.

Alieleza kuwa lengo kuu la kambi hiyo ni kuweza kugundua wagonjwa wa saratani walio katika hatua za awali ili waweze kupata matibabu kwa wakati na kuweza kurahisisha rufaa za wagonjwa wa saratani kuweza kufika katika taasisi ya saratani ya ocean road bila usumbufu ikiwa ni pamoja na kubadilishana uzoefu kwa madaktari kati ya Taasisi ya ocean road ,hospitali ya rufaa ya Mkoa ya mount meru pamoja na hospitali ya selian juu ya magonjwa ya saratani.

Dkt.Maguha aliongeza kuwa lengo lao katika kambi hiyo ni ili kuweza kugundua saratani katika hatua za awali za saratani ambazo zinatibika na kuweza kupunguza wagonjwa ambao wanakuja katika hatu zilizo kubwa za ugonjwa huo.

Sambamba na hayo amebainisha njia za kuweza kujikinga na ugonjwa wa saratani ikiwa ni pamoja na kuenenda na mtindo bora wa maisha kwa maana ya ulaji zaidi wa vyakula vya mbogamboga na matunda,kuepuka ula wa mafuta mengi ya wanyama,kuepuka kula vyakula vyenye ukingu ambayo ni kihatarishi cha kupata saratani ya ini.

"Katika hilo tunashauriwa kuweza kufanya zoezi ya mara kwa mara ili kujiepusha na magonjwa haya ya saratani pamoja na magonjwa mengine yasiyoambukiza,kuepuka uzito uliokithiri,kupunguza matumizi ya pombe kupita kiasi sambamba na kujiepisha na matumizi ya tumbaku maana mambo haya yote ni tabia hatarishi ambazo zinaweza zikatuweka katika hatari ya kupata magonjwa ya saratani."alieleza Dkt.Maguha Stephano

Ameongeza kwa kuwashauri watanzania kuweza kupima afya zao mara kwa mara na kupata chanjo ya homa ya ini huku akiwataka wazazi na walezi kuwapekeka watoto wao wa kike wenye umri wa miaka 9 hadi 14 katika vituo vya afya ili kuweza kupatiwa chanjo huku akiwataka pia kuondokana na imani potofu kuwa chanjo hiyo ina madhara kwa mabinti zao.

Pamoja na hayo jumla ya wanawake 351 waliweza kufanyiwa vipimo vya saratani ya matiti na mlango wa kizazi ambapo kati ya hao wanawake 7 walikutwa na mabadiliko ya awali ya saratani ya mlango wa kizazi,4 wakiwa na viashiria vya saratani ya mlango wa kizazi na 9 wakiwa na vivimbe katika matiti ambapo utafiti unaendelea kufanyika kubaini kama ni saratani ili waweze kupatiwa matibabu zaidi.

Katika zoezi hilo pia wanaume waliojiyokeza kupima saratani ya tezi dume idadi yao ilikuwa 100 ambapo kati yao wanaume 7 walikutwa na viashiria vya saratani ya tezi dume ambapo nao wapo katika uchunguzi ili waweze kuanza matibabu kama watagundulika kuwa na ugonjwa huo.Share To:

Post A Comment: