Na Elizabeth Joseph, Monduli.


HALMASHAURI ya Wilaya ya Monduli imetakiwa kuhakikisha fedha zote za mapato ambazo bado hazijawekwa Benki zinawekwa mara moja kama ilivyoshauriwa na Mkaguzi wa ndani ili kudhibiti upotevu wa fedha hiyo.

Kauli hiyo ilitolewa Katibu Tawala Msaidizi,Ufuatiliaji wa Menejimenti na Ukaguzi Mkoa wa Arusha Bw,Ramadhan Madeleka wakati wa kikao cha Baraza la kawaida la Madiwani wa Halmashauri hiyo kilicholenga kujadili taarifa za Kata na kusema Halmashauri hiyo imekuwa chini kwenye ukusanyaji wa mapato ambapo hadi sasa imekusanya karibu asilimia 52 tofauti na uhalisia uliotakiwa hadi sasa kukusanya kuanzia asilimia 68 huku fedha nyingi zikiwa bado mikononi mwa watu na nyingine kutowekwa Benki.

"Mfano katika taarifa ya Mkaguzi wa ndani imeonesha kiasi Cha shilingi Milioni 112 ambazo zilikusanywa hazijapelekwa Benki huku shilingi Milioni 138 zikionesha hazijakusanywa kutoka kwenye vibanda"alisema Katibu Tawala huyo.

Aliongeza kuwa taarifa ya Mkaguzi huyo pia imeonesha jumla shilingi Milioni 83 hazijakusanywa kutoka kwa wafanyabiashara kwa kutolipia leseni za biashara.

"Lakini Mkaguzi wa ndani kaainisha pia wafanyabiashara 47 hawajalipa ushuru wa huduma,serikali tayari ilishaingia makubaliano na TRA kwamba kila Halmashauri unakwenda kuchukua Return za wafanyabiashara na hizo ndizo zitawasaidia kukusanya service leavy halisi"aliongeza kusema Bw,Madeleka.

Aidha aliwataka Madiwani na Wataalam wa Halmashauri hiyo kuhakikisha wanashirikiana ili kuhakikisha lengo la Bajeti waliyoiweka linafanikiwa kwakuwa lengo kubwa la Mkoa ni kuhakikisha kila Halmashauri inafikia lengo hadi inapofikia Juni 30.

Hata hivyo awali akijitambulisha katika Baraza hilo Mkuu wa Wilaya ya Monduli Mh Joshua Nassari aliwaomba Madiwani na Watumishi wa Halmashauri kushirikiana kwa pamoja kuangalia namna bora ya kuboresha mapato ikiwa ni pamoja na kuangalia changamoto zilizopo katika ukusanyaji wa mapato ili kuzitatua pamoja.

"Ni aibu mno unafika mwisho wa mwaka wa fedha mmakuta mpo asilimia 60 ya mapato ya Halmashauri,Wilaya hii ni kongwe na ina heshima yake hivyo lazima tuongeze asilimia ya mapato yetu na kwenye hili tutakuwa serious na asijitokeze mtu kutukwamisha katika hili"alisisitiza Mkuu wa Wilaya hiyo.

Share To:

Post A Comment: