************************

Azma ya Serikali ya jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kuhakikisha kuwa nchi inajitosheleza katika uzalishaji wa mchele ili kupunguza matumizi makubwa ya fedha kuagiza mchele kutoka nje ambapo mpaka sasa tunategemewa na nchi jirani katika zao la mchele kwani sisi ndio tunazalisha kwa wingi.

Ameyasema hayo Katibu Tawala wa Wilaya ya Kahama Mhe.Timoth Ndanya wakati akifungua mafunzo kwa wajasiriamali-wazalishaji wa bidhaa za mchele kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya hiyo leo Mei 31,2022.

Amesema kutegemewa katika uzalizaji wa zao la mchele ni pamoja na kwenda sambamba na uzalishaji wa mchele unaozingatia viwango, ubora na usalama ili kulinda afya ya mlaji na zaidi kuongeza soko la mchele katika nchi jirani.

"Tukijibidiisha katika uzalishaji wa namna hiyo kutaifanya nchi yetu kujenga uchumi endelevu wenye nguvu, imara na wenye ushindani". Amesema Mhe.Ndanya.

Aidha Mhe.Ndanya amesema kuwa mafunzo hayo yatalenga kutoa elimu kwa wajasiriamali ambao ni wachakataji, na wafungashaji wa mchele pamoja na wadau wengine katika uzalishaji wa zao la mchele, kuhusu kanuni bora za uzalishaji, matakwa ya viwango, namna bora ya uhifadhi, elimu juu ya vifungashio na taarifa za msingi zinazotakiwa kuwepo kwenye vifungashio pamoja na teknolojia ya uchakataji wa mchele.

"Uongozi wa Wilaya unaamini kuwa mafunzo haya ni njia muafaka ya kuleta tija zaidi katika juhudi za kuliletea taifa letu maendeleo ya haraka kulingana na fursa zilizopo hasa kwenye sekta ya viwanda, kilimo, biashara, uvuvi na maeneo mengine mengi". Amesema

Pamoja na hayo ameishukuru Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kwa maandalizi ya mafunzo haya muhimu na ninaomba utaratibu wa kufanya mafunzo kama haya uwe endelevu.
Share To:

emmanuel mbatilo

Post A Comment: