Julieth Ngarabali  ,Bagamoyo. 


Mkuu wa Mkoa Pwani Abubakar Kunenge amewataka watalaamu wa afya Mkoani humo kutumia  utaalamu wao na kuja na Mikakati mizuri ili kupata matokeo mazuri ya kupunguza vifo vya mama na mtoto wakati na baada ya kujifungua.


Kunenge ameyasema hayo  akifungua kikao kazi cha Wataalamu na Wadau wa Utekelezaji wa Mradi wa afya ya mama na mtoto unaotekelezwa na shirika la Afya la Korea Foundation for International  health Care ( KOFIH ) huko Wilayani Bagamoyo mkoani humo.


Amesema kupitia mradi huo wa KOFIH Mkoa huo umeweza kupunguza vifo vya akina mama vitokanavyo na uzazi kitoka 82 mwaka 2015 hadi 51 mwaka 2021 na vya watoto wachanga vimepungua kutoka 887 mwaka 2015 hadi 392 mwaka 2021.


Kunenge amewataka Wataalamu hao kushirikisha Wananchi katika uandaaji wa mipango yao.


"Lazima mjipange muumize  vichwa kweli kweli ili tupate mikakati yenye matokeo chanya katika kupunguza vifo vya mama na mtoto ' amesema Kunenge na kuongeza


 "Matarajio yanafahamika katika Sera na ilani ya Chama cha Mapinduzi nini kifanyike kufikia malengo hayo kwa hiyo ni kazi yenu sasa ninyi Wataalamu" Pia Kunenge amewashukuru wadau hao kuongeza mwaka mmoja wa Mradi huo  kwenye Halmashauri sita na kufanya kuwa wa miaka saba na wameongeza kiasi cha pesa toka dola za kimarekani 3,000,000 hadi  dola 4,900,000.


Awali akizungumzia faida mbalimbali zilizotokana na mradi wa KOFIH Mganga Mkuu Mkoani Pwani, Dk. Guni Kamba amesema wameweza kupata mafunzo mbalimbali ikiwemo ya Wataalam watoa dawa za usingizi, Ujenzi wa vyumba vya upasuaji, vifaa tiba, ambulance na kujengewa wadi za wagonjwa,


Naye mwakilishi wa Wizara ya Afya  Dk .Phineas  Sospiter  ameshukuru utekelezaji mradi huo kwa sababu unaisadia pia Wzara hiyo kuendelea kupiga hatua mbele katika kupunguza vifo vya mama na mtoto.


Aidha  Mwakilishi wa KOFIH Tanzania Mr Seungrae Ha  amesema kwa pamoja wameweza kukuza huduma za Afya Tanzania, na wamekutana kwenye kikao hicho kufanya tathimin ya mradi huo kwa miaka sita iliyopita na kupanga mipango ya Utekelezaji kwa mwaka ujao.


Kikao hicho kilihudhuriwa na madaktari Wakuu wa Wilaya,  timu za usimamizi wa Afya za Wilaya, wawakilishi kutoka Mikoa ya  Pwani, Dodoma na Morogoro.


Share To:

JUSLINE

Post A Comment: