KAIMU Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof.James Mdoe,akizungumza na waandishi wa habari leo Desemba 3,2022 jijini Dodoma kuhusu dhamira ya kukuza lugha ya Kiswahili  kwenye mataifa mengine kwa kupandisha bango Mlima Kilimanjaro lenye kauli mbiu isemayo ‘Kiswahili Kileleni’ kama sehemu ya maadhimisho ya miaka 61 ya Uhuru.

Na Alex Sonna-DODOMA

WIZARA ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imedhamiria kukuza na kueneza Lugha ya Kiswahili kimataifa kwa kupandisha bango maalumu Mlima Kilimanjaro lenye  ujumbe wa kukitangaza Kiswahili kimataifa.

Hayo yamesemwa leo Desemba 3,2022 Jijini Dodoma na Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Prof.James Mdoe, amesema watatumia maadhimisho ya miaka 61 ya uhuru kuhamasisha matumizi ya lugha ya Kiswahili Duniani ambapo kwa sasa mataifa mengi yanahamasika kutumia lugha ya Kiswahili.

“Lengo la kufanya hivyo ni kusherehekea Uhuru wa Taifa letu kwa kutangaza Lugha ya kiswahili Kwa mataifa mengine ndio maana bango hili litapandishwa na kusimikwa katika kilele cha Mlima Kilimanjaro kama ambavyo ulisimikwa Mwenge wa uhuru,”

 “Wameandaliwa vijana wawili shupavu ambao watakwenda kusimika Bango lenye kauli mbiu “Kiswahili Kileleni” kwenye kilele Cha mlima Kilimanjaro siku ya maadhimisho ya miaka 61 ya Uhuru wa Tanzania,”Amesema Prof.Mdoe

Hat hivyo ameeleza  kuwa kwa sasa takribani watu milioni 250 ulimwenguni wanazungumza lugha ya Kiswahili na ukizingatia Shirika la umoja wa mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni UNESCO tayari imeitambua lugha ya Kiswahili na kuitengea siku maalumu ambayo ni July 7 kila mwaka.

“Ukizingatia Kiswahili ni Lugha ya kwanza kutambuliwa na UNESCO na kukitengea siku maalumu na sisi kama Wizara ya Elimu tunawajibu kwa kuendelea kukitangaza Kiswahili zaidi kimataifa” amesema.

Hata hivyo, amesema lugha ya Kiswahili kwa sasa inapendwa na watu wengi na kuzungumzwa ikiwamo nchini Misri ikiwa moja katika ya nchi inayofundisha lugha ya Kiswahili tangu mwaka 1964.

“Kuna vyuo 150 vinafundisha Kiswahili, pia  redio na runinga 300 ulimwenguni ambazo zinarusha vipindi kwa lugha hiyo hapo ni nje ya Vyuo vya hapa nchini pia  vyuo vya Tanzania vina makubaliano na vyuo vya nje kwa ajili ya kuendelea kufundisha lugha hii na tayari mikataba minne imeingiwa na Wizara.”

“Tunaendelea na mazungumzo na wizara hizo za nje ya nchi yakikamilika mikataba mingine mitano itasainiwa ili kuwezesha uanzishwaji wa madarasa ya kufundishia lugha hiyo nchini,” amesema.

Aidha amebainisha kuwa kwa sasa nchi jirani na Tanzania zinazungumza lugha ya Kiswahili  nchi hizo ni kama Uganda, Kenya, Sudani Kusini, Malawi na Mashariki ya Kongo.

“Na hivi juzi tu kwa kushirikiana na ubalazi wa Tanzania nchini Malawi  tumefungua darasa la kufundisha lugha ya Kiswahili  Malawi na tumekuwa tukisisitiza Mabalozi wetu wote kuzungumza na nchi husika” amesema.

Aidha ametoa wito kwa Mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania katika Mataifa mbalimbali kuendelea kuchochoe matumizi ya Lugha ya kiswahili katika mataifa hayo ikiwemo kufungua madarasa ya awali ya kufundisha Lugha ya kiswahili.

Kwa upande wake Mwalimu wa Lugha ya Kiswahili na mwandishi wa vitabu kwa lugha ya Kiswahili Menna Yasser raia wa Misri amesema Kiswahili kinanafasi kubwa kwa mataifa mbalimbali ni muhimu kuendelea kukitangaza zaidi.

“Hii ni lugha ambayo mataifa mengi yanatumia, kuna umuhimu wa kukuza lugha ya Kiswahili, hii lugha imenipa fursa nyingi na nimeisomea,” amesema.

Naye, mtunzi  wa mashairi kwa lugha ya Kiswahili Meja Mwinyikombo Ally ameipongeza Wizara ya Elimu kwa kubuni njia hiyo kukitangaza Kiswahili na kuamini kuwa Kiswahili ni kama bidhaa inayouzika nchini na nje ya nchi.

 

KAIMU Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof.James Mdoe,akimsikiliza Mwalimu wa Lugha ya Kiswahili na Mwandishi wa vitabu kwa lugha ya Kiswahili Menna Yasser raia wa Misri akielezea umuhimu wa Kiswahili katika mataifa mbalimbali ni muhimu kuendelea kukitangaza zaidi.

MTUNZI wa Mashairi kwa lugha ya Kiswahili Meja Mwinyikombo Ally,akiipongeza Wizara ya Elimu kwa kubuni njia hiyo kukitangaza Kiswahili katika Mataifa ya nje.

 

KAIMU Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof.James Mdoe,akiwakabidhi vijana wawili shupavu bango lenye kauli mbiu “Kiswahili Kileleni” kwenye kilele Cha mlima Kilimanjaro siku ya maadhimisho ya miaka 61 ya Uhuru wa Tanzania.

 

KAIMU Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof.James Mdoe,akiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kutoa taarifa kuhusu dhamira ya kukuza lugha ya Kiswahili  kwenye mataifa mengine kwa kupandisha bango Mlima Kilimanjaro lenye kauli mbiu isemayo ‘Kiswahili Kileleni’ kama sehemu ya maadhimisho ya miaka 61 ya Uhuru.


Share To:

Post A Comment: