Mkurugenzi wa kituo cha kulea watoto yatima na wanaoishi kwenye mazingira magumu  cha  Goodwill and Humanity Foundation Muhzari Muhammad kilichopo jijini Tanga.

Na Denis Chambi, Tanga. 

Vitendo vya ukatili kwa watoto vimeendelea kuongezeka kila kukicha licha ya jitihada zinazofanyika kuvitokomeza huku wazazi walezi na jamii kwa ujumla wakitajwa kuwa chanzo kwa kushindwa kutoa ushirikiano kwenye mamlaka za kisheria mara wanapoyaona matukio hayo kwenye mazingira wanayoishi. 

Hayo yamebainishwa na afisa ustawi wa halmashauri ya jiji la Tanga Stela Mbugi wakati wa kusherehekea kutimiza miaka saba kwa kituo cha kulea watoto yatima na wanaoishi kwenye mazingira magumu cha Good will and humanity Foundation ambapo ameeleza kuwa kwa asilimia kubwa watoto wamekuwa wakifanyiwa vitendo vya ukatili na watu wao wakaribu huku wazazi wakitajwa kumalizana na watuhumiwa kwa kigezo cha kulipwa fedha ili wasiende kuripoti ngazi za kisheria. 

"Hali sio nzuri sana kwa sababu wakati mwingine hawa watu wanaofanya ukatili ni watu wa karibu, hawa watu wengine wa mbali sio ziada lakini ukifwatilia kwa kina wazazi wenyewe wanahusika moja kwa moja inapofika kwenye ufwatiliaji wa kesi kuna watuhumiwa wanatoroshwa na wanamalizana na mzazi anakubali apewe pesa ilibasiende kutoa taarifa polisi" 

"Nomba sana ushiriki wa wazazi na walezi kutoa taarifa juu yq vitendo hivi , kwa sasa hivi inaonekana mkoa wa Tanga unashika namba tatu kati ya mikoa kumi katika ukatili hii inaonyesha wazi kama taarifa zingekuwa zinatolewa matukio yangeweza kuisha kabisa au kupungua naomba tushirikiane na tuwe mfano wa kuwaibua wale wanaofanya ukatili "alisema Stella. 

Alisema kuwa lipo wimbi kubwa la watoto waliopo chini ya miaka kumi wanaofanya biashara za kuuza karanga na kahawa ndani ya jiji la Tanga wengi wao wakitokea wilaya ya Lushoto ambapo inaonekana kuna mtandano wa utumikishwaji wa watoto wazazi na walezi wakiwatumia kama sehemu ya kujipatia kipato. 

"Watoto wengi ambao tunawaona sasa hivi ni wakutoka ndani ya wilaya zetu sana sana wilaya ya Lushoto wengi wanakuja kuuza Karanga idara yetu ya ustawi wa jamii tumekuwa tukiwarudisha lakini baada ya muda mfupi unawakuta katika mazingira mengine , nitoe rai kwa wazazi na walezi wasiwafanyishe watoto wao biashara lakini wale ambao wanawafanyisha watoto biashara hizi waache hiyo tabia"

 Awali akizungumza mkurugenzi wa kituo cha Goodwill and Humanity foundation Muhzari Muhammad ameiasa jamii kuendelea kuwa na moyo wa kujitoa kwaajili ya watu wenye mahitaji mbalimbali ikiwemo kulitazama kundi la watoto ambalo limekuwa likikubwa na adha mbalimbali ikiwemo ukatili huku akiwaomba viongozi wa dini kutumia nafasi zao katika kuelimisha jamii hasa katika maswala ya kiimani.

 "Sisi kama taasisi tunatambua na kuthamini watu wanaoishi kwenye mazingira magumu tuiombe jamii iweze kuyatambua makundi kama haya na kuyasaidia lakini tuwaombe sana viongozi wa dini katika maeneo mbalimbali hapa nchini waweze kutumia nyumba zao za ibada kukemea vitendo vya ukatili kwa watoto lakini serikali iendelee kuwachukulia hatua kali wahusika ili tuweze kukomesha na kutokomeza janga hili" alisema Muhammad.

 Kwa upande wake mwenyekiti wa taasisi ya Shujaa wa maendeleo na ustawi wa jamii Tanzania 'SMAUJATA' wilaya ya Tanga Said Mmasa amesema kuwa katika kuendelea kuadhimisha siku 16 za kupinga ukatili kwenye jamii hasa kwa watoto wameendelea kutoa elimu kwa jamii ambapo wamefanikiwa kuzifikia kata mbalimbali za jiji la Tanga.

 "Tumeingia kila kata kila mtaa kuhamasisha na kutoa elimu kwamba siku 16 hizi tunapunguza ukatili dhidi ya watoto, tumeripotiwa matukio mengi ya ukatili na sasa tunashirikiana bega kwa bega na jeshi la polisi kuwapeleka watuhumiwa kwenye mkono wa sheria na pia kuhakikisha kuwa haki za watoto tunazisimamia , tumeanza utaratibu maalumu wa kuwafuata wazazi kwamba wawaangalie watoto tukijua kuwa wao ndio walezi wa kwanza wa watoto," alisema Mmasa 

Aidha ameongeza kuwa SMAUJATA imekuja na mpango kabambe wa kutoa elimu kwa wazazi na walezi kwa kutambua kuwa ukatili umeonekana ukiinza kukua kutoka ngazi ya familiya.
Share To:

Post A Comment: