Na Mwandishi wetu, Dodoma

WAKATI Serikali ikihaha kutafuta vyanzo vipya vya mapato ikiwa ni pamoja na kuanzisha tozo mbalimbali ambazo zimekuwa zikilalamikiwa na wananchi, imeelezwa kuwa Sh bilioni 64. 3 zimetafunwa kwenye Bandari ya Tanga, baada ya kutolewa kwa zabuni iliyogubiwa na utata kila kona.

Ufisadi huo umeibuliwa na Mbunge wa Viti Maalumu CCM, Judith Kapinga, wakati akichangia taarifa ya ukaguzi maalumu wa Mthibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG),  iliyowasilishwa bungeni na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC).

Kapinga akichangia taarifa hiyo ya CAG inayoishia Februari 2022, alisema ufisadi katika bandari hiyo ulitokana na mkataba wa mwaka mmoja ambao Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Nchini (TPA), iliingia na  Kampuni ya China Harbour Engineering Company (CHEC) wa Sh bilioni 172.36.

Alisema mkataba huo uliingiwa Agosti 3 mwaka 2019 na ulipaswa kuisha Agosti 2020, ambapo ulilenga kuongeza kina cha lango na sehemu ya kugeuzia meli katika Bandari ya Tanga, kufanya tathmini ya athari za kimazingira, na kununua vifaa kwaajili ya shughuli za bandari.

Alisema kwa mujibu wa mkataba huo, gharama ya kuongeza kina cha lango na sehemu ya kugeuzia meli katika Bandari ya Tanga ilikuwa ni Sh bilioni 104.92 fedha ambayo ni asilimia 60 ya mkataba wote.

Kapinga alisema, Agosti mosi 2019 Kampuni ya CHEC iliuza kazi hiyo kwa mkandarasi mbia, ikiwa ni siku mbili kabla ya kampuni hiyo ya China haijasaini mkataba na Mamlaka ya Bandari.

Alisema baada ya kampuni hiyo kutoa kazi siku moja kabla ya kusaini mkataba na TPA, siku mbili baadaye yaani Agosti 3, ilisaini rasmi mkataba na Mamlaka ya Bandari wa kufanya kazi hiyo kwa Sh bilioni 104.92, ili hali tayari CHEC ilishatoa kazi hiyo kwa mkandarasi mbia kwa Sh bilioni 40.

“Kampuni ya CHEC yaani China Harbour Engineering Company alipewa kazi hiyo kwa Sh bilioni 104.92, hakufanya ila aliigawa kwa bei rahisi kwa mkandarasi mbia, kwa mkataba  wa dola za marekani milioni 18.15 sawa na Sh bilioni 40.46 kwa kipindi cha miezi 11 bila kutoa taarifa kwa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari. 

“Piamkandarasi mkuu kampuni ya CHEC yaani China Harbour Engineering Company aliingia mkataba na ‘mkandarasi Mbia’ hata kabla ya kusaini mkataba wake na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kwakuwa walisaini  Agosti mosi 2019 kabla ya Mkataba wa Mkandarasi Mkuu na TPA, Agosti 3, 2019,” alisema. 

Alisema kuingia mkataba bila kutoa taarifa kwa Mamlaka ya Bandari ilikuwa ni kinyume na Kifungu Kidogo cha 4.4 cha masharti ya jumla ya mkataba kati ya Mamlaka ya Bandari na mkandarasi mkuu ambacho kinazuia mkandarasi mkuu kutoa sehemu ya kazi kwa mkandarasi mwengine.

Alisema kwa mujibu wa kifungu hicho, ikiwa kunauhitaji wa kutoa kazi kwa kampuni  nyingine kutekeleza kazi zilizoko kwenye mkataba, mkandarasi  mkuu anapaswa kutoa taarifa kwa Mamlaka ya Bandari siku 28 kabla  ya kutoa kazi hiyo.

Kwa mujibu wa Kapinga, CAG alibaini, jumla ya malipo yaliyolipwa kwa kazi ya kuongeza kina cha lango na sehemu ya kugeuzia meli yalikuwa dola za marekeni milioni 18.22 sawa na Sh  bilioni 40.62, kiasi hiki, pia, kinajumuisha malipo ya dola za marekani 73,824 sawa na Sh  milioni 164.55 kwa huduma za wakala wa meli kwa mkandarasi mbia. 

Alisema ulinganifu wa kiasi kilichotozwa na mkandarasi mkuu cha Sh bilioni 104.92 na kiasi alicholipwa na mkandarasi mbia cha Sh bilioni 40.62 inaonesha kiasi kilichotozwa na mkandarasi mkuu kimezidi kiasi halisi kilichotumika kufanya malipo ya kazi hiyo kwa Sh bilioni 64.30.

#TPA ilitoa kazi kwa kampuni ya kachina kwa Sh bilioni 104.92, wakati kampuni ikiuza kazi hiyo kwa Sh bilioni 40 siku mbili kabla haijasaini mkataba na Mamlaka ya Bandari 



Share To:

Post A Comment: