Naibu Waziri wa Kilimo Mh.Anthony Mavunde ametoa rai kwa watendaji wa serikali kuhakikisha yale maeneo yote ambayo migogoro ya ardhi imetatuliwa yanapangiwa mipango ya matumizi ya ardhi kwa kujumuisha maeneo ya mashamba makubwa ya kilimo badala ya kupanga maeneo ya makazi tu peke yake.

Naibu Waziri Mavunde ametoa kauli hiyo jana wàkati akizungumza na wananchi wa kijiji cha Lyamidati mkoani Shinyanga wakati Kamati ya Mawaziri nane wa Wizara za Kisekta wanaoshughulikia migogoro ya matumizi ya ardhi ya vijiji 975 walipofika eneo hilo.

"Nitoe rai yale maeneo ambayo migogoro yake ya matumizi ya ardhi imetatuliwa basi iwekewe matumizi bora ya ardhi   ili mashamba makubwa yasisahaulike na wakulima wapate maeneo ya kutosha walime mwisho wa siku waisaidie nchi kukuza uchumi wao mtu mmoja mmoja,uchumi wa kaya na taifa kwa ujumla.

Badala ya maeneo ambayo utatuzi wake umefanyike kutengwa kwa ajili ya makazi peke yake ni lazima wataalamu wasimamie mipango ya matumizi bora ya ardhi kwa kuhakikisha wanaingiza maeneo makubwa ya mashamba ya kilimo kwa sababu Mh Rais Samia Suluhu Hassan amekuja na mpango wa kuwa na mashamba makubwa ya pamoja(_block farms_) ili kusaidia kukuza sekta ya kilimo kufikia malengo yake ya kukua kwa asilimia 10 ifikapo mwaka 2030.

Mashamba haya makubwa ya pamoja yatasaidia kurahisisha utoaji wa huduma za ugani kwa wakulima hasa katika mbinu bora za kilimo cha tija na usambazaji wa teknolojia mbalimbali za kilimo ili kusaidia kuongeza uzalishaji wa mazao ya kilimo, serikali ina mpango wa kuwa na mashamba makubwa ya pamoja 10000 kufikia mwaka 2030 na kubainisha kuwa, kwa sasa hivi nchi nzima ina jumla ya mashamba makubwa ya pamoja zaidi ya 110”

Kamati ya Mawaziri nane wa Wizara za kisekta iko katika ziara ya kutembelea mikoa mbalimbali kwa lengo la kutoa mrejesho wa Maamuzi ya Baraza la Mawaziri kuhususiana na utatuzi wa migogoro ya matumizi ya ardhi katika vijiji 975 na tayari katika awamu hii ya pili kamati hiyo imeshatembelea mikoa ya Rukwa, Katavi, Kigoma, Simiyu na Shinyanga.





Share To:

Post A Comment: