TUME ya Utumishi wa Walimu (TSC) imetakiwa kuwachukulia hatua walimu wanaokiuka maadili, vitendo vya utovu wa nidhamu na kudhibiti utoro.

Imeelezwa kuwa utoro ni asilimia 66.5 ya makosa ya walimu.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Tamisemi, Dk Festo Dugange alitoa maelekezo hayo jijini hapa jana wakati akifungua mkutano wa kwanza wa Baraza la Walimu nchini.

Dk Dugange alisema kwa kuwa kosa la utoro kwa walimu linaongoza kwa asilimia 66.5, viongozi wanapaswa kufuatilia kosa hilo ili kujua sababu.

“Naomba TSC fuatilieni suala hili la utoro. Hatuhitaji kuona walimu wanatoroka, badala yake wafanye kazi,” alisema.

Kuhusu utatuzi wa changamoto za walimu, Dk Dugange alisema serikali inazifanyia kazi ili ziweze kutatuliwa.

Pia aliitaka TSC kuendelea kutoa mafunzo ya Tehama kwa walimu katika mikoa yote huku akiagiza kupeleka vifaa hivyo vya Tehama katika mikoa minne ambayo imefanyiwa majaribio.

Naye Katibu TSC, Paulina Nkwama alisema wao kama Tume wanajitahidi kusimamia makosa mbalimbali yakiwemo ya nidhamu ambapo alisema walimu wamekutwa na makosa 11,366 ambapo asilimia 66.5 wamekutwa na kosa la utoro.

Makosa mengine ni kughushi vyeti, walimu 1,438 sawa na asilimia 33.5, uhusiano kimapenzi walimu na wanafunzi 328, ulevi 89 na uzembe 56.

Share To:

Post A Comment: