Na Christina Thomas, Morogoro


WAJASIRIAMALI mkoani hapa wamemuomba Rais Samia Suluhu Hassan kuendelea kuwashika mkono wanawake wajasiriamali kwa kuihamasisha jamii kununua bidhaa zinazozalishwa ndani ya nchi ili kuwainua kiuchumi.


Mmoja wa Wajasiriamali hao kutoka ZARADI Group Zaituni Diwa alisema hayo kwenye maonesho ya 46 ya siku ya wakulima 88 Kanda ya Mashariki yaliyofanyika kwenye viwanja vya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere yakihusisha mikoa ya Morogoro, Dar es salaam, Tanga na Pwani  alisema wakiwa watano kwenye kikundi chao huzalisha viungo mbalimbali na kupata wateja wachache kutoka ndani na nje ya nchi.


Diwa alisema wajasiriamali huzalisha bidhaa nzuri na bora kwa afya lakini masuala ya masoko bado yamekuwa changamoto kwao kwa sababu watanzania kupenda bidhaa za nje.


Naye Meneja wa Shirika la kuhudumia viwanda vidogo (SIDO) mkoani hapa Joan Nangawe  alisema wajasiriamal wamekuwa wakikumbwa na changamoto ya masoko ya ndani na nje na kwamba kama SIDO wanajitahidi kuwatafutia masoko na kuwakumbusha kanuni ya kukaa pamoja kibiashara ili kuwavutia wateja. 


Hivyo aliwashauri wajasiriamali kuhamasika na kununua viwanja katika maeneo ya pamoja yaliyotengwa na Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro na kujenga ili kuepukana na changamoto ya kukosa maeneo makini ya ujenzi wa miundombinu ya kuchakata bidhaa zao.


Nangawe alisema wajasiriamali wengi wanakumbana na changamoto ya maeneo ya kufanyia kazi lakini wakiitumia vyema fursa hiyo kwa kununua viwanja kwenye maeneo yaliyotengwa kata za Kiegeya na Tungi na kujenga miundombinu inayokidhi vigezo na viwango itawasadia kukuza uchumi wao.


Hata hivyo alisema SIDO mkoa inawakaribisha wajasiriamali kupanga katika eneo la viwanda vidogovidogo la SIDO lililopo kata ya Kihonda Mbuyuni ambapo viwanja hupandishwa kwa gharama nafuu kwa kujenga viwanda vya kudumu au sio vya kudumu kulingana na mkataba watakaoingia ili kusaidia wajasiriamali wasikose sehemu ya kufanyia kazi.


Alisema pia wana mkakati wa kutengeneza sehemu ambayo wajasiriamali watatumia mindombinu ya kufanya uzalishaji na kwamba mjasiriamali atakwenda na malighafi zake na atazalisha na kuondoka na bidhaa zake.


Meneja huyo alisema SIDO hutoa huduma za teknolojia na ubunifu, maendeleo ya biashara na mafunzo, masoko na uwekezaji na huduma za fedha ambapo aliwataka wajasiriamali kuitumia nafasi ya mikopo inayotolewa kupitia SIDO pekee na kwa kushirikiana na Taasisi za huduma za kifedha.



Nangawe alisema huwa wanatoa mafunzo kwa kila mwaka kwa wajasiriamali 2000 wakiwemo mtu mmoja mmoja, vikundi au makundi yanayoletwa na Taasisi au miradi.


Hivyo aliwataka wajasiriamali kujitokeza kupata mafunzo ili kurasimisha biashara zao na kuweza kulipa kodi, kupata tenda na kushiriki kwenye maonesho mbalimbali na kupata masoko.

Share To:

Post A Comment: