Waziri wa Habari mstaafu, Dk.Harrison Mwakyembe.

 

 

Na Mwandishi Wetu

 

MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), imeombwa kuchukua hatua dhidi ya Kalomba online TV ambayo imekuwa na mwenendo mbaya wa kuchafua viongozi na kuwasingizia kifo na hivyo  kuzusha taharuki kwa jamii.

TV hiyo ya mtandao mwishoni mwa wiki iliyopita  ilimzushia kifo Waziri wa Habari mstaafu, Dk.Harrison Mwakyembe kwamba amefariki dunia.

"Kuanzia Jumamosi kuamkia Jumapili iliyopita kuna taarifa zilizokuwa zikisambazwa kwanza kwa simu na 'message' za kawaida kuwa nimefariki dunia kesho yake zikaanza kurushwa kwenye TV ya mtandao iitwayo Kalomba TV kwa kutumia picha zangu mbili tofauti," alisema Dk.Mwakyembe.

Dk. Mwakyembe akizungumza na Blog hii,  hakukana wala kukubali kulihusisha tukio hilo na njama za kisiasa kwani lilianza kusambazwa siku ya ziara ya Rais wa Jamhuri wilayani Kyela.

Alisema kuwa taarifa hiyo ya Kalomba TV imesababisha mtafaruku mkubwa kwenye familia yake ambapo watoto wake na baadhi ya ndugu zake wa karibu waliumia kisaikolojia na wengine kupata shinikizo la damu.

"Nahisi waliopanga njama hiyo walitaka nipokelewe kwenye mkutano wa Rais kwa nderemo na mhemko mkubwa na pengine hata kuvuruga kwa muda mkutano wa Rais halafu baadaye nisingiziwe kuwa nilitengeneza mwenyewe taarifa hiyo ya msiba ili nipokelewe na wananchi kwa hisia kali”, alisema.

Aliongeza kuwa kwa bahati chale zikamcheza, akaamua kurudia njiani.

Dk.Mwakyembe ambaye alikuwa waziri katika wizara mbalimbali ikiwemo ya Habari, alishamtaarifu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia,Nape Nauye, kuhusu suala hilo naye akaahidi kulifanyia kazi.

Tazama hapa chini chapisho la kalomba onlineTv.
Share To:

dottomwaibale

Post A Comment: