.....................

Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Zanzibar (THRDC-Zanzibar) unaendesha mafunzo kwa maafisa wa jeshi la polisi, maofisa kutoka ofisi ya mwendesha mashtaka mkuu wa serikali (DPP) pamoja na maofisa kutoka Chuo cha Mafunzo (Magereza) Zanzibar.

Kwa mujibu wa taarifa ambayo imetolewa leo na Afisa Habari THRDC imesema Mafunzo hayo  ya siku mbili yameanza leo Augosti 24, 2022 katika ukumbi wa Golden Tulip Hotel, Mjini Unguja huku mgeni rasmi akiwa ni Kamishna wa jeshi la polisi Zanzibar, Mh. Hamad Khamis Hamad.

Aidha mafunzo hayo yamelenga kukuza uelewa wa maswala ya haki za binadamu na kuwakumbusha maofisa wa jeshi la polisi, mawakili kutoka katika ofisi ya mwendesha mashtaka mkuu wa serikali pamoja na maofisa wa chuo cha mafunzo (Magereza)  kuendelea kufanya kazi kwa kufuata misingi ya haki za binadamu na kujadili changamoto zilizopo hususani za ukatili wa kijinsia pamoja na ukatili wa watoto ili kushauriana namna bora ya kutatua na kuondokana na changamoto hizo.

Mafunzo hayo yameandaliwa kutokana na uwepo wa ongezeko la vitendo vya ukatili wa kijinsia visiwani Zanzibar ambapo kwa kipindi cha mwezi Januari hadi Juni, 2022 jumla ya kesi 487 za udhalilishaji ziliripotiwa, ukilinganisha na kesi 634 za udhalilishaji zilizoripotiwa kwa mwaka 2021, jambo linalopelekea jeshi la polisi pamoja na mamlaka mbali mbali kuhakikisha jitihada za ziada zinafanyika ili kumaliza kabisa changamoto hizo.

Mafunzo hayoni mwendelezo wa juhudi zinazofanywa na mtandao katika kuhakikisha wadau mbali mbali wa haki za binadamu hasa maofisa watekelezaji sheria wanafanya kazi kwa kufuata misingi ya haki za binadamu hasa katika utekelezaji wa majukumu yao pindi wanapohudumia wananchi.

Share To:

Adery Masta

Post A Comment: