Na Bakari Madjeshi, 
SIMBA  Day 2022 ni ya 14 kufanyika tangu kuasisiwa na kina Mzee Hassan Dalali (Field Marshal) mwaka 2009, Tamasha la mwaka huu limekuwa la kufana na kukonga nyoyo za wengi nchini hususani wadau mbalimbali wa soka.

Kilele cha Simba Day kila mwaka kinafanyika katika dimba la Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam, huku Wasanii mbalimbali nchini wakitumbuiza sanjari na matukio, maonyesho mbalimbali kutoka kwa Wasanii na hata Watoto wadogo.

UWANJA WA BENJAMIN MKAPA WAFURIKA
Tamasha hilo mwaka huu limefanyika Agosti 8, 2022, ijapokuwa siku ya sikukuu ya Nane Nane, tamasha lilipendezeshwa na Mashabiki lukuki waliojaza uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, Mashabiki hao wameitwa na wameitika kushuhudia Wachezaji wao wapya waliosajiliwa kwa ajili ya msimu ujao wa mashindano wa 2022-2023.

Licha ya Mashabiki wa Simba SC kuujaza uwanja huo walipewa zawadi ya ushindi wa bao 2-0 dhidi ya St. George ya Ethiopia, licha ya kuujaza uwanja huo, baadhi ya Mashabiki wa upande wa pili, Watani wa Jadi, Yanga SC walihudhuria tamasha hilo pia.

BURUDANI KUTOKA KWA WASANII MBALIMBALI
Kwenye tamasha hilo kulikuwa na Wasanii wengi lakini Msanii kutoka Lebo ya WCB, Zuhura Othman maarufu Zuchu ametia ‘Fola’ kwenye tamasha hilo, kwa hakika! amekonga nyoyo za wengi baada ya kuingia kwa kushuka na Kamba kama Askari, bila shaka wengi hawakuamini kama angeweza kuingia uwanjani kwa kutumia Kamba.

Mara ya mwisho wadau na mashabiki wa soka kushuhudia Msanii kushuka na Kamba na kuingia uwanjani ilikuwa tukio la Siku ya Mwananchi misimu miwili iliyopita, ambapo Msanii Harmonize kutoka Lebo ya Konde Gang alifanya hivyo akiwa amevalia vazi la kijeshi.

Pia tumeshuhudia ubunifu wa Simba SC katika kushawishi Watoto wadogo (Vijana) kuipenda timu hiyo ya Wekundu wa Msimbazi, Watoto hao walionyesha halaika na kuunda maumbo mbalimbali yanayoihusu timu hiyo, wakipambwa na ‘Brass Band’ ya Jeshi la Polisi nchini.

Watoto hao wa halaiki walionyesha ubunifu kwa kuunda maumbo mbalimbali, yakiwemo maumbo yanaonyesha ‘Slogan’ za Simba SC, ikiwemo ile ya Nguvu Moja, Ahsante MO Dewji na mengine mengi.

KAGERE, LWANGA WAANGWA MBELE YA MASHABIKI
Aliyekuwa Mshambuliaji wa timu hiyo, Meddie Kagere na Kiungo Mkabaji, Taddeo Lwanga rasmi wameangwa na timu hiyo mbele ya Mashabiki lukuki wa timu hiyo, baada ya Wachezaji hao kufika makubaliano ya pande mbili kuachana na Simba SC hivi karibuni.

Kagere na Lwanga wameagwa vizuri na timu hiyo huku wakipewa zawadi kutokana na utumishi wao katika Kikosi hicho kwa muda wote waliokuwa hao, hata hivyo wote wameshukuru Wanasimba na kuwatakia kila la kheri katika safari yao ya msimu ujao.

USHINDI WA BAO 2-0 DHIDI YA ST. GEORGE
Simba SC hawakutaka kuharibu sherehe hiyo iliyohudhuriwa na idadi kubwa ya Mashabiki wa Soka, Wekundu wa Msimbazi wametoa dozi ya bao 2-0 dhidi ya St. George SC ya Ethiopia katika mchezo wao wa kirafiki.

Wachezaji wa wapya waliosajiliwa na Klabu hiyo, wakiwepo pia Wachezaji wa kigeni walionyesha kiwango bora zaidi na kuchagiza ushindi huo wa mabao 2-0 dhidi ya Wahabeshi hao kutoa Ethiopia, kwenye siku hiyo muhimu kwa Wanasimba.

Mabao mawili yaliyofungwa na Mshambuliaji Kibu Dennis (Kibu D) kipindi ch kwanza, dakika ya 18 na Nelson Okwa kipindi cha pili, dakika ya 59 ya mchezo. Licha ya ushindi huo, timu ya Wanawake, Simba Queens nao walipata ushindi wa bao 2-0 dhidi ya Fountain Gates Princess.
Share To:

Post A Comment: