Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Bwana Sahili Geraruma amewataka wananchi wa kata ya Olirien Wilayani Ngorongoro kuunganisha Maji katika nyumba zao pindi mradi utakapo kamilika.


Ameyasema hayo pindi Mwenge ulipokuwa akitembelea na kukagua mradi wa Maji katika kata ya Olirien.


"Wananchi wakiunganisha Maji kwenye nyumba zao itasaidia kumtua mama ndoo Kichwani na upatikanaji wa Maji utakuwa wakutosha kwa matumizi ya nyumbani".


Aidha, bwana Geraruma amewataka wataalamu wa Mamlaka ya Maji safi na usafi wa mazingira Ngorongoro (RUWASA) kukamilisha mradi huo kwa wakati ili wananchi waweze kupata Maji kwa wakati.


Akisoma taarifa ya mradi huo Meneja wa RUWASA Ngorongoro Mhandisi Gerald  Andrew amesema, mradi huo hadi kukamilika kwake utagharimu zaidi ya Milioni 583, ambazo ni fedha za Serikali kutoka mpango wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa ustawi wa Taifa na mapambano dhidi ya UVIKO 19.


Mradi huo ni upanuzi na uendelezaji wa skimu ya kupeleka huduma ya Maji katika Hospitali ya Wilaya ya Ngorongoro, na ujenzi ulianza Januari 2022 na unatarajiwa kukamilika Juni 30,2022.


Amesisitiza kuwa mradi huo unatarajia kuhudumia wananchi takribani 7000 na mifugo 8000 katika vijiji vya Lopolun,Olirien na Oldonyowas pamoja na shule ya msingi Lemishiri, Oldonyowas na hospitali ya Wilaya.


Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2022  ulipokelewa rasmi Mkoani Arusha Juni 20 kutoka Mkoa wa Manyara na unatarajiwa kukabidhiwa Mkoani Mara mnamo Juni 27.
Share To:

Post A Comment: