![]() |
Moja ya mabasi ya wanafunzi likiwa njiani kwenda kuchukua ili kuwapeleka shuleni |
Na Abby Nkungu, Singida
SERIKALI imeombwa kutoa mwongozo kwa
shule binafsi juu ya muda maalum wa kuwapitia majumbani wanafunzi wa elimu ya
awali kwa ajili ya kuwapeleka shule ili kuwalinda watoto hao pamoja na
kutowaathiri kimasomo, kiafya, kiakili na kisaikolojia.
Ombi hilo lilitolewa kwa nyakati tofauti na baadhi ya wazazi na walezi
katika Manispaa ya Singida wakati wakizungumzia utekelezaji wa Programu
Jumuishi ya Taifa juu ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT-
MMMAM) ya miaka mitano iliyoanza mwaka 2021- 2026.
Walisema kuwa pamoja na Programu hiyo kuonesha mafanikio kwa kushughulikia
masuala mtambuka kwa mtoto aliye chini ya miaka minane, bado ipo changamoto ya
watoto wa shule za awali kwenye shule binafsi kuchukuliwa mapema asubuhi kuliko
kawaida hali inayoweza kuwaathiri kiafya na kielimu.
“Mimi mtoto wangu wa chekechea anapitiwa na gari la shule saa 11 alfajiri,
hivyo ili kumuandaa inabidi nimuamshe saa 10:30 kwani kuna muda wa kusumbuana hadi aamke na
nimbembeleze aache kulia kwa usingizi ndipo nimuogeshe na kumvalisha nguo”
alisema Elibariki Mollel, mmoja wa wazazi eneo la Minga, Manispaa ya Singida.
"Kuna siku mtoto wangu alirejea nyumbani akiwa na jeraha kwenye paji
la uso. Nilipomhoji akaniambia alijigonga kwenye gari asubuhi wakati anaenda
shule kwa vile alikuwa anasinzia" alilalamika Mollel na kuongeza kuwa
tatizo ni uchache wa magari kwenye shule husika hivyo kulazimika kutoka mapema
kuzunguka mji mzima wakifuata wanafunzi hadi saa 2:00 asubuhi ndipo wanaingia
darasani.
Mzazi mwingine, Hussein Njenje alisema kutokana na changamoto hiyo
amelazimika kutafuta nyumba ya kupanga jirani na shule wanakosoma wajukuu wake
ili kuwaondolea adha ya kufuatwa alfajiri na gari hali inayoweza kuwaathiri
kiafya watoto kwa kutopata usingizi wa kutosha lakini pia inaweza kusababisha
waichukie shule kwa kuona kama vile hiyo ni adhabu kwao.
Mmoja wa walimu katika shule binafsi
ambaye hakupenda kutajwa jina lake ili
kulinda ajira yake, alikiri kuwa kitendo cha watoto wa chekechea kuamshwa
mapema kila siku kinawaathiri kiafya na
kielimu.
“Siku moja wewe njoo pale shuleni kwetu saa 4:00 asubuhi baada ya kunywa
uji. Utaona huruma kwani utakuta
asilimia kubwa ya watoto wanachapa usingizi na
wengine walio macho wanapiga miayo tu kwa usingizi na uchovu baada ya
kuzungushwa mji mzima kwa gari kabla ya kuingia darasani “ alieleza mwalimu
huyo.
Ingawa Kaimu Ofisa elimu msingi Manispaa ya Singida, Siah Mtafya
alikiri kuwa kuwachukua wanafunzi wa
awali alfajiri sana sio utaratibu mzuri, lakini alisema kuwa hakuna sheria, kanuni wala Mwongozo wa
Serikali unaoelekeza muda muafaka wa kuwapitia wanafunzi hao kuwapeleka shule.
Hata hivyo, alisema kuwa watakaa na Uongozi wa shule husika ili kuona namna
bora ya kushughulikia suala hilo muhimu.
Naye Kaimu Kamanda wa Polisi mkoa wa Singida, ACP Lucas Mwakatundu alisema
kuwa hakuna utaratibu wa muda uliowekwa wa kuanza safari asubuhi mabasi ya
shule kama ilivyo kwa mabasi ya abiria kwani majukumu yake yanafanana sana na
mabasi ya wafanyakazi (staff buses); hivyo ni vigumu kuchukua hatua za kisheria.
Hata hivyo, wakati wenye Mamlaka wakibainisha kuwa hakuna sheria wala
mwongozo, Daktari Bingwa mshauri wa magonjwa ya wanawake na watoto katika
Hospitali ya Rufaa mkoa wa Singida, Dk Suleiman Muttani alieleza kuwa mtoto
chini ya miaka minane anatakiwa kulala kwa muda wa saa 9 hadi 10 kwa siku.
Alisema kuwa iwapo watoto wa darasa la awali watalala saa 2:00 au 3:00
usiku na kuamshwa kila siku saa 11 alfajiri au kabla ya hapo kwenda shule,
wanaweza kupata madhara kiafya; ingawa nafuu ipo kwa shule zenye utaratibu wa
kuwapa fursa ya kulala kwa muda ili kuwapunguzia usingizi.
Kwa mujibu wa PJT- MMMAM, Tanzania ni nchi ya kwanza katika ukanda wa Afrika Mashariki kuifanya elimu ya awali kuwa ya lazima kwenye Sera ya elimu na mafunzo ya mwaka 2014 ili kuijumuisha elimu ya awali katika elimu za msingi kwa kuzitaka shule zote kuwa na darasa la elimu ya awali kwa watoto walio na umri chini ya miaka mitano.
Post A Comment: