Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI), chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii, imeandaa Kongamano la 15 la Kimataifa la Kisayansi, litakalowakutanisha wanasayansi zaidi ya 500 litakalofanyika tarehe 3-5 Desemba 2025, katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Arusha (AICC), hapa jijini Arusha.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi hiyo Dkt. Eblate Mjingo, ofisini kwake Jijini Arusha, alipokuwa akizungumza na Wanahabari. 

Dkt. Mjingo amebainisha  lengo la Kongamano hilo ni kurejesha matokeo ya tafiti zinazofanywa na TAWIRI pamoja na wadau wake kwa Serikali, Mamlaka za Uhifadhi, Wadau wa Uhifadhi, na watanzania wote. 

"Matokeo haya yatatumiwa na watunga sera na wafanya maamuzi kwa ajili ya kuhakikisha uhifadhi na utalii endelevu nchini Tanzania, na duniani kwa ujumla". Alisema Dkt. Mjingo.

Aidha ameongeza kuwa mada kuu ya kongamano hilo ni ‘Ubunifu katika uhifadhi wa wanyamapori na Utalii endelevu: Kutafuta mustakabali katika ulimwengu unaobadilika’ au “Innovations in Wildlife Conservation and Sustainable Tourism: Navigating the Future in a Changing World”.

Naye Mkurugenzi wa Utafiti TAWIRI Dkt. Julius Keyyu amesema kuwa, nchi zaidi ya 20 zinatarajiwa kushiriki kongamano hilo huku huku mawasilisho 248 kuwasilishwa pamoja na  kuwa na maonesho ya matokeo ya tafiti mbalimbali.
Share To:

Post A Comment: