Mbunge wa zamani wa Jimbo Ngorongoro Mhe. Kaika Saning'o Ole Telele akielezea  utayari wake wa kuhama kwa hiari kwenda Kijiji cha Msomera Handeni Mkoani Tanga.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. John Mongela akizungumza na waandishi wa Habari jkuelezea zaidi ya kaya 25 kutoka ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro zinazotarajiwa kuhama kwa hiari kwenda Kijiji cha Msomera Wilaya ya Handeni Mkoani Tanga wiki hii alhamis tarehe 30 juni, 2022


 Na Mwandishi wa NCAA, Arusha.


Mbunge wa zamani wa Jimbo Ngorongoro Mkoani Arusha Mhe. Kaika Ole Telele amebainisha kuwa yuko tayari kuhama kwa hiyari kwenda Kijiji cha Msomera Wilaya ya Handeni Mkoani Tanga kuungana na wananchi wengine ambao wameshahamia.

Mhe. Telele ambaye aliwahi kuwa Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi katika Serikali ya awamu ya nne ameeleza kuwa ameamua kufanya maamuzi hayo ili kupunguza shughuli za kibinadamu ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro.

“Nimeona ni kweli idadi ya watu na mifugo ndani ya Hifadhi imeongezeka, nimehamasika baada ya kuona zoezi hili ni la hiari na Serikali yetu imeboresha miundombinu muhimu kule Msomera Handeni, mimi binafsi nimetafakari na kwa hiari yangu mwenyewe nimeamua kuondoka ili wengine nao waendeleee kuhamasika na kuunga mkono zoezi hili muhimu ambalo linaendeshwa kwa amani na utulivu kabisa” alifafanua Mhe. Telele.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. John Mongela ameeleza kuwa zaidi ya kaya 25 kutoka ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro zinatarajia kuhama kwa hiari kwenda Kijiji cha Msomera Wilaya ya Handeni Mkoani Tanga wiki hii alhamis tarehe 30 juni, 2022.

Mhe. Mongela ametoa kauli hiyo leo tarehe 27 juni, 2022 wakati akiongea na waandishi wa Habari katika ofisi za Makao makuu ya NCAA Karatu Mkoani Arusha kuelezea tathmini ya utekelezaji wa zoezi hilo la Wananchi wanaoendelea kujiandikisha kwa hiari.

Amebainisha kuwa zoezi la wananchi kujiandikisha linaendelea vizuri kwa amani na usalama ambapo kundi hilo la tatu lenye familia zisizopungua 25 linajumuisha wananchi na viongozi wa kimila wanaoishi ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro.


Share To:

Post A Comment: